Sumu yaua watoto 400 Nigeria | Habari za Ulimwengu | DW | 06.10.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Sumu yaua watoto 400 Nigeria

Kwa mujibu wa Chama cha Madaktari wasiokuwa na Mipaka, MSF, watoto 400 wamefariki kutokana na sumu inayotoka kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wadogo Kaskazini mwa Nigeria.

Watoto wa Kinigeria, ambao wako katika hatari ya kuambukizwa kutokana na sumu ya madini ya risasi kutoka kwenye machimbo ya dhahabu

Watoto wa Kinigeria, ambao wako katika hatari ya kuambukizwa kutokana na sumu ya madini ya risasi kutoka kwenye machimbo ya dhahabu

Vifo hivi vinaripotiwa kutokea ndani ya kipindi cha miezi sita tu iliyopita, katika vijiji kadhaa vya jimbo la Zamfara, ambapo chembechembe za madini ya risasi kutoka kwenye mashimo ya uchimbaji haramu wa dhahabu zimeuchafua udongo na maji ya eneo hilo.


Mkurugenzi wa Mradi wa MSF, El-Shafii Muhammad Ahmad, amesema kwamba kutokana na rekodi za vifo vinavyohusiana na sumu hii, huenda idadi halisi ya watoto waliofariki inazidi hapo. Taarifa za mwanzo zilizochapishwa jana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa zinasema kwamba idadi ya watoto wanokufa kwa sumu hii inazidi kuongezeka.


'Migodi' ya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu nchini Nigeria

'Migodi' ya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu nchini Nigeria

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusiana na Misaada ya Kibinaadamu mjini Geneva, Elisabeth Byrs, aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba, zaidi ya watoto 3,000 wanaishi katika vijiji saba vilivyoathiriwa na sumu hiyo katika eneo ambalo lina uchimbaji mkubwa wa ovyo ovyo wa dhahabu.


Byrs alisema kwamba uharibifu wa mazingira katika eneo hilo ni wa kiwango cha juu na hautarajiwi kumalizika kwa haraka na wazazi wengi wanaogopa kusema pale watoto wao wanapouguwa maradhi yanayotokana na sumu na badala yake huchukulia kwamba watoto hao wanaumwa na maradhi mengine kama vile malaria.


Wazazi hawa pia wanaficha tatizo halisi lililopo kwa kuwa wanaogopa serikali inaweza kupiga marufuku shughuli zao za uchimbaji wa dhahabu, ambazo kwao zina faida kubwa zaidi ya kiuchumi kuliko kilimo.


Katika eneo hili, wanawake na watoto hujishughulisha na shughuli za utengenezaji wa madini ya risasi yanayotumika kusafisha dhahabu na kawaida huchukua vipande vya madini ya risasi majumbani kwao, ambapo nako watoto huweza kuvuta hewa au kunywa maji yaliyochanganyika na sumu hii.


Hata hivyo, Mtaalamu wa Maradhi ya Kuambukiza wa Serikali ya Nigeria, Henry Akpan, ameikana idadi ya vifo hivi vya watoto iliyotolewa na MSF akisema kwamba imetiwa chumvi. Ingawa alikataa pia kutaja idadi ambayo serikali inayo, lakini alisema kwamba hakujakuwa na vifo vipya kwa wiki za hivi karibuni. Alisema kwamba sasa serikali inatoa huduma nzuri zaidi za kitabibu kwa watoto, wajawazito na wale walioathirika na maambukizi ya sumu hizi.


Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba idadi ya vijiji vinavyochafuliwa na sumu hizi inazidi kuongezeka katika eneo lote la Kaskazini Magharibi ya Nigeria lenye shughuli nyingi za uchimbaji madini.

Hatari ya maambukizi haya huwa inajitokeza siku nyingi baada ya kiwango kikubwa cha madini ya risasi kujengeka mwilini na kusababisha maumivu makali yasiyo ya kawaida, kuufelisha ukuwaji wa mfumo wa fahamu na hatimaye kuathiri mafigo na kusababisha kifo.


Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman


DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com