Nigeria: Uhuru, umasikini na matumaini | Habari za Ulimwengu | DW | 28.09.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Nigeria: Uhuru, umasikini na matumaini

Tarehe 1 Oktoba, Nigeria inaadhimisha miaka 50 ya uhuru wake, huku nchi hiyo yenye wakaazi wengi kabisa barani Afrika, ikikabiliwa na changamoto nyingi.

Rais Jonathan Goodluck wa Nigeria. Nchi yake inatimiza miaka 50 ya uhuru

Rais Jonathan Goodluck wa Nigeria. Nchi yake inatimiza miaka 50 ya uhuru

Sherehe nyingi zinapangwa kufanyika katika maadhimisho ya Oktoba 1, ikiwemo ile ya kukatwa keki kubwa kabisa duniani, lakini wachunguzi wanasema Nigeria bado inaendelea kukabiliwa na matatizo makubwa yanayotishia mustakabali wake, ikiwemo kutapaka kwa njaa, ufisadi, vurugu za kidini na serikali inayoshindwa kutimiza ahadi zake, licha ya kwamba nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mafuta.

Uchimbaji wa nchini Nigeria. Licha ya taifa hili kuzalisha mafuta kwa wingi, bado inatajwa kuwa miongoni mwa nchi masikini duniani

Uchimbaji wa nchini Nigeria. Licha ya taifa hili kuzalisha mafuta kwa wingi, bado inatajwa kuwa miongoni mwa nchi masikini duniani

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaona dalili za matumaini katika taifa hili linaloshikilia nafasi ya kwanza kwa idadi ya watu barani Afrika, ikiwemo mwamko wa wapiga kura dhidi ya utawala wa kifisadi na utayarifu wao wa kusisitiza mabadiliko. Wengine wanautaja ushawishi wa utamaduni wa nchi hii, ambayo imezalisha waandishi na wanamuziki wenye majina makubwa duniani kama vile Fela Kuti, Chinua Achebe na Wole Soyinka, aliyekuwa Mwafrika wa kwanza kupokea tunzo ya Nobel kwa kazi zake za fasihi.

Nigeria ni nchi ambayo pengo baina ya masikini na matajiri ni kubwa sana, ambapo mabanda ya madongo-kuporomoka yamejengwa kuzunguka majumba ya kifakhari katika ilivyo kwenye jiji la Lagos. Pamoja na kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta, taifa hili la Afrika Magharibi linashikilia nafasi ya 158 kati ya nchi 182 zenye viwango duni vya afya, elimu na hali ya maisha.

Lakini ukwasi na ufukara ni mstari mmoja tu wa utengano nchi hii. Nigeria inatajwa kama nchi moja yenye mataifa mengi. Raia wake milioni 150 wamegawika baina ya Wakristo na Waislam kutoka makabila 250 tafauti. Hata uchaguzi wa Januari mwakani unakabiliana na ukweli huu. Watu wengi katika chama tawala wanataka Muislam kutoka Kaskazini ndiye agombee urais na sio Rais wa sasa, Jonathan Goodluck ambaye ni Mkristo wa Kusini na ambaye ameshatangaza nia yake ya kugombea.

Jambo hili linawatia watu khofu kwamba nchi hii hivi sasa ipo njia panda na kwamba kosa dogo tu linaweza kuigeuza kuwa Somalia ya Afrika ya Magharibi. Ndivyo anavyoona mchumi na mgombea urais kutoka upinzani, Pat Utomi.

"Ila wacha nitarajie kwamba tutapiga mayowe, tutagombana kwa maneno, lakini mwisho tutaandama njia iliyo sawa na Nigeria itakuwa kigezo chema kwa nchi nyengine." Anasema Utomi.

Juu ya yote, ukweli kwamba Nigeria imemudu kuendelea kuishi kama taifa moja kwa nusu karne nzima, licha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1967 hadi 1970, mkururo wa mapinduzi ya kijeshi, na mapigano ya kidini, ni jambo linalotosha kuwafanya Wanigeria wastahiki hongera za kutimiza miaka 50 ya uhuru.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com