Sudan kukatiza mahusiano na Korea Kaskazini | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sudan kukatiza mahusiano na Korea Kaskazini

Marekani imesema kwamba nchi ya Sudan itakata mahusiano yote ya kijeshi na kibiashara na Korea Kaskazini.

Ni hatua ambayo huenda ikawa ushindi mkubwa wa juhudi za utawala wa Trump za kulitenga taifa hilo la Asia  licha ya kuzidi kwa mvutano kufuatia majaribio ya silaha za nyuklia na makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani Heather Nauert alisema Sudan inachukua hatua hiyo kutokana na "tishio kubwa" linalotokana na mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Alisema Marekani imekaribisha uamuzi huo, uliotangazwa baada ya ziara ya naibu waziri wa mambo ya nchi za kigeni John Sullivan mjini Khartoum.

Ziara hiyo ilikuja wakati Marekani na Sudan, zikihimizwa na Israeli na Saudi Arabia, wakielekea kuimarisha  mahusiano bora zaidi baada ya miongo kadhaa ya uadui.

"Kuitenga serikali ya Korea Kaskazini ni kipaumbele kwa Marekani, na ni kipengele muhimu cha kudumisha amani na utulivu duniani kote," Nauert alisema katika taarifa.

"Marekani inaishukuru Sudan kwa kutimiza ahadi ya kuchukua hatua hizi muhimu kwa sababu ya kitisho kikubwa kinachosababishwa na" Korea ya Kaskazini.”

Utawala wa Trump umekuwa ukizitia msukumo  nchi za kigeni kukata mahusiano ya kiuchumi, kidiplomasia na mengine na Korea Kaskazini katika jitihada za kuitenga nchi hiyo na kuirudisha kwenye meza ya majadiliano.

Katika wiki za hivi karibuni, utawala huo umekuwa ukiyalenga mataifa ya Kiafrika na Kusini mwa Asia na kadhaa wamekubaliana.

Sudan imekuwa mtazamo maalum wa juhudi hiyo kama sehemu ya jaribio la kuboresha uhusiano kati ya Marekani na Sudan, ambayo ilisababisha kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya Marekani  dhidi ya Sudan.

Huku Korea ya Kaskazini ikiendelea kutengwa na mataifa ya magharibi, nayo imezidi kutafuta mahusiano na mataifa ya Afrika, Mashariki ya Kati na kusini mwa Asia ili kukusanya fedha zinazohitajika.

Nordkorea Kim Jong Un bei Besuch einer Fabrik für Nuklearwaffen (Reuters/KCNA)

Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akitoa mwelekeo kwenye mpango wa silaha za nyuklia

Barani Afrika, imeimarisha uhusiano wa kijeshi na kiuchumi na nchi kadhaa, ikiwa Sudan, Uganda na Angola, kwa kutoa mipango ya mafunzo ya kijeshi, ujenzi na miradi ya viwanda na usambazaji wa wafanyakazi wageni.

Mwezi uliopita, Uganda ilitangaza kuwa imewaondoa wataalam wa kijeshi wa Korea Kaskazini na wawakilishi wa makampuni ya ya Korea Kaskazini, ikiwa ni pamoja na muuzaji wake mkuu wa silaha, kama sehemu ya jitihada za kuzingatia vikwazo vipya vya umoja wa mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini kwa miaka mingi imekuwa ikiwapa mafunzo wanajeshi wa  Uganda ,ya vita vya bahari na utunzaji wa silaha.

Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika, alijibu tangazo la Sudan kwa kusema Umoja wa Afrika umeshutumu uenezaji  wa silaha za nyuklia katika bara hilo na mahali pengine.

"Maendeleo na utengenezaji wa silaha hizi inakuwa tishio la kweli kwa amani na usalama duniani," mkuu huyo wa AU alisema katika mahojiano na shirika la habari la  AP.

Tangazo hili la Alhamisi lilikuja kabla ya uamuzi uliotarajiwa hivi karibuni kwa Marekani  kuiorodhesha tena Korea ya Kaskazini kama "serikali inayodhamini ugaidi," jina ambalo liliondolewa na utawala wa Rais George W. Bush mnamo mwaka wa 2008 kwa kuwa ulitaka makubaliano ya kidiplomasia kuzuia mpango wa silaha za atomiki wa Korea kaskazini.

Msemaji wa ikulu ya White House Sarah Huckabee Sanders aliwaambia waandishi wa habari kwamba anatarajia uamuzi juu ya hali ya Korea Kaskazini kuamuliwa mapema wiki ijayo.

Sudan ni moja ya nchi tatu tu - nyingine ni Iran na Syria - ambazo kwa sasa zimeteuliwa wafadhili wa ugaidi na wizara ya nchi ya kigeni, jina linalobeba vikwazo vya uchumi na kifedha. Tangazo la Sudan kukata mahusiano na Korea ya Kaskazini kunaweza kusaidia kesi yake kuondolewa kutoka kwenye orodha hiyo.

Hata hivyo, afisa wa wizara ya mambo za kigeni alisema uwezekano wa mabadiliko ya uteuzi ya Sudan na Korea Kaskazini hauhusiani na kwamba ukaguzi wa nchi zote mbili unaendelea.

Afisa huyo, ambaye hakuwa na mamlaka ya kuzungumza jambo hilo kwa umma na aliyezungumza katika hali ya kutojulikana, alisema uamuzi juu ya Sudan unaweza kutegemea jinsi itakavyotelekeza ahadi yake ya kukata mahusiano na Korea Kaskazini.

Taarifa ya Nauert ilisema Marekani  "itaendelea kushirikiana juu ya suala hili ili kuhakikisha kuwa ahadi hii imetekelezwa kikamilifu."

Mwandishi: Fathiya Omar/APE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com