Shinzo Abe azuru Pearl Harbour kwa mara ya kwanza | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Shinzo Abe azuru Pearl Harbour kwa mara ya kwanza

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, awasili Hawaii. Abe na mwenyeji wake rais Barack Obama wanatrajiwa kushiriki kwenye kumbukumbu ya kuwaenzi mabaharia na wanamaji waliokufa kwenye mashambulio katika bandari ya Pearl.

Shinzo Abe ndiye waziri mkuu wa kwanza wa Japan kuhudhuria sehemu ya kumbukumbu ya USS Arizona. Eneo hilo litafungwa kwa umma kwa ajili ya ziara hiyo ya Abe na mwenyeji wake Rais Barack Obama, ambaye yumo likizoni katika mji huo wa Hawaii pamoja na familia yake. 

Ziara ya Abe ni baada ya ile ya Obama kuuzuru mji wa Hiroshima nchini Japan akiwa ndiye rais wa kwanza wa Marekani kufanya hivyo. Hiroshima ni mji ambao Vita vya Pili vya Dunia vilikomalizikia na ziara ya Abe katika eneo vilikoanzia vita hivyo ni ya kihistoria na inayolenga kuonesha uhusiano ulioimarika baina ya nchi hizo mbili.

Ni miaka 75 tokea tukio la Pearl Harbor

Baada ya miaka 75 tangu Wajapani walipofanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo yaliitumbukiza Marekani katika Vita vya Pili vya Dunia, viongozi hao watakutana leo hii Honolulu, mji mkuu wa jimbo la Hawaii, katika kisiwa cha Oahu kilicho katikati ya Bahari ya Pasifiki. 

USA Abe gedenkt als erster japanischer Regierungschef der Opfer von Pearl Harbor (picture alliance/dpa/MAXPPP)

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, akiwakumbuka wanajeshi wa Kimarekani waliouawa

Abe na Obama watazuru mabaki ya manowari ya kivita ya USS Arizona ambamo mabaharia 1,177 pamoja na wanamaji walikufa. Mabaki ya manowari hiyo bado yanaonekana mpaka leo.  Mnamo tarehe 7 mwezi Desemba mwaka 1941, rais wa Marekani wakati huo, Franklin D. Roosevelt, alitangaza kuwa Jenerali Isoroku Yamamoto, wa Japan aliamuru mashambulizi mabaya katika eneo la Bandari ya Pearl. Shambulizi hilo lilikuwa la kushtukiza. Majeshi ya Japan yalizizamisha na kuziharibu manowari za kivita za Marekani. Wamarekani 2,403 waliuwawa na wengine 1,100 walijeruhiwa. Manowari ya kuhifadhia silaha ya USS Arizona pia iliripuliwa.

Mtaalamu wa maswala ya Japan katika Taasisi ya Maswala ya Kigeni ya Marekani, Shella Smithi, anasema ziara hiyo inaazimia kutafuta fursa za kufungua mazungumzo baina ya Marekani na Japan juu ya mambo yaliyopita na vita hivyo kwa jumla. Smith anasema kuwa fursa kama hiyo itafungua uwezekano mkubwa wa kutafuta maridhiano ambayo ni muhimu.

Alipozuru Hiroshima mwezi wa Mei katika uwanja uliojengwa Mnara wa Amani wa Hiroshima, Rais Obama aliandika ujumbe kwenye kitabu cha wageni uliosema: "Tumejua machungu yanayosababishwa na vita. Hebu sasa tujitahidi kwa pamoja kuendeleza amani na tujitahidi kuwa na dunia isiyo na silaha za kinyuklia."

Bandari ya Pearl na Hiroshima ni sehemu zinazoashiria mwanzo na mwisho wa vita baina ya Marekani na Japan. Mkutano wa viongozi hao wawili unafanyika huku zikiwa zimebakia wiki nne tu kabla ya kuapishwa rais mteule wa Marekani, Donald Trump.   

 

Mwandishi: Zainab Aziz/AFP


Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com