1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali Uingereza yashindwa kesi ya Brexit

Iddi Ssessanga
24 Januari 2017

Mahakama ya juu nchini Uingereza imesema waziri mkuu Theresa May laazima apate idhini ya bunge kabla ya kuanzisha mchkatao wa nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya maarufu Brexit.

https://p.dw.com/p/2WKG2
Großbritannien Karikatur zum Brexit vor dem Obersten Gericht in London
Picha: picture-alliance/dpa/V. Jones

"Leo, kwa wingi wa majaji 8 kwa watatu, mahakama inahukumu kwamba serikali haiwezi kuanzisha kipengele cha 50 bila sheria ya bunge inayoiruhusu kufanya hivyo," alisema Jaji David Neuberger wakati akisoma huku hiyo.

Katika hukumu hiyo mahakama ilisema muswada kama huo, ambao unatarajiwa kupelekwa bungeni ama baadae wiki wiki au wiki ijayo, unaweza kuwa mkataba mfupi sana.

Mara baada ya kutolewa hukumu hiyo waziri anaehusika na Brexit David Davis, alisema serikali itawasilisha sheria ya waziwazi ndani ya siku chache kutaka idhini ya bunge kuanzisha mchakato huo.

"Tutawasilisha ndani ya siku chache, muswada wa sheria kuipa serikali mamlaka ya kisheria kuanzisha kipengele cha 50 na kuanza mchakato rasmi wa kujiondoa," alisema waziri Davis bunge na kuongeza kuwa, huu ndiyo utakuwa muswada wa wazi zaidi iwezekanavyo kutekeleza uamuzi wa watu na kuheshimu hukumu ya mahakama ya juu.

Großbritannien Gina Miller Urteil des Obersten Gerichts zu Brexit
Gina Miller, mwanaharakati aliefungua shauri mahakani kutaka bunge liwe na usemi katika kuanzisha mchakato wa Brexit.Picha: Getty Images/L. Neal

Fursa kwa wabunge

Uamuzi huo  wa mahakama unaweka njia kuuchambua mchakato huo, wabunge ambao wengi wao walitaka Uingereza ibakie katika Umoja wa Ulaya. Hata hivyo chama kikuu cha upinzani cha Labour kilisema hakitazuwia Brexit ingawa kitajaribu kuifanyia marekebisho sheria hiyo.

Taarifa za vyombo vya habari zimesema hadi wabunge 80 wa Labour katika bunge hilo la wajumbe 650 watapuuza matamshi hayo yaliotolewa na kiongozi wa chama chao Jeremy Corbyn, na kupiga kura dhidi ya kuanzisha mchakato huo, huku chama kidogo cha Liberal Democratic kimesema kitapinga mchakato mzima wa Brexit isipokuwa iitishwe kura ya pili ya maoni kuhusu makubaliano ya mwisho.

Wakati huo waziri kiongozi wa Scotland Nicolas Sturgeon ameibua uwezekano wa kura nyingine ya uhuru wa Scotland baada ya mahakama hiyo kuamua kwamba bunge la Scotland halihitaji kushauriwa kuhusu kuanzisha mchakato wa Brexit.

Kura mpya ya uhuru Scotland?

"Nadhani ni suala la kanuni za kidemokrasia kwamba bunge la Scotland linapaswa kuwa na usemi katika suala kubwa kama hilo lenye athari kubwa iwapo linakubaliana au hapana kuhusu kuanzishwa kipengele cha 50," alisema Sturgeon katika mahojiano mjini Edinburg.

Großbritannien General Jeremy Wright Rede nach dem Urteil zu Brexit
Mwanasheria mkuu wa Uingereza Jeremy Wright akitoa taarifa baada ya mahakama kutoa hukumu yake.Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

"Nadhani hapa kuna suala la msingi: Je tunafurahia kuruhusu mustakabali wetu kuamuliwa na serikali mjini Westminster yenye mbunge mmoja tu nchini Scotland au ni wakati kwetu kujiamulia mustakabali wetu?"

Wascotland walikataa kuwa huru mwaka 2014, lakini chama tawala cha Sturgeon cha Scottish National Party SNP, kinasema uamuzi wa Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya mwezi Juni dhidi ya matakwa ya wapigakura wa Scotland, umeweka mazingira ya kura nyingine ya maoni kuhusu uhuru.

Baadhi ya wawekezaji na wale waliounga mkono Uingereza kubakia katika Umoja wa Ulaya wanatumai wabunge watamlaazimu waziri mkuu May kutafuta makubaliano yanayotoa kipaumbele kwa ushirikia wa nchi hiyo katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya linalohudumia watu milioni 500 au hata kuzuwia kabisa mchakato huo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.

Mhariri: Daniel Gakuba