1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia Suluhu aapishwa kuwa rais wa Tanzania

John Juma na Hawa Bihoga
19 Machi 2021

Aliyekuwa makamu wa rais wa Tanzania bi Samia Suluhu Hassan ameapishwa rasmi leo Ijumaa kuwa rais wa Tanzania.

https://p.dw.com/p/3qqWL
Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha urais
Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha uraisPicha: Stringer/REUTERS

Samia mwenye umri wa miaka 61 ameapishwa kuchukua wadhifa huo baada ya kifo cha Rais John Pombe Magufuli.

Yeye ndiye mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini Tanzania. Samia ameapishwa leo Ijumaa katika ikulu ya jijini Dar es Salaam.

Kwenye taarifa, ikulu imesema Samia Hassan ataongoza kikao cha baraza la mawaziri baada ya kulihutubia taifa.

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan atahudumu kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa urais hadi pale uchaguzi mwingine wa urais utakapofanyika.

Punde baada ya kula kiapo na kukagua gwaride lililoambatana na mizinga ikiwa ni utaratibu wa kawaida kama amri jeshi mkuu, analihutubia taifa kwa kuanza kutoa taratibu za mazishi ya hayati Rais Magufuli ambapo maombolezo yatakuwa ni siku 21 na ataanza kuagwa katika jiji la Dar es Salaam na kufuatiwa na mikoa mingine ambayo imechaguliwa na serikali ili kuwakilisha mikoa yote na kisha kuzikwa nyumbani kwao Chato kama ambavyo alisisitiza marehemu.

Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la kijeshi
Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la kijeshiPicha: Stringer/REUTERS

Mfahamu zaidi Samia Suluhu

Katika ratiba hiyo pia Rais huyo wa kwanza mwananmke katika ukanda wa afrika mashariki, amelitangazia taifa lake siku mbili za mapumziko ya kitaifa ikiwemo siku ya kuaga wananchi wa dodoma na siku ya maziko ambayo ni machi 25.

Aidha katika kuliweka taifa sawa, amewataka raia wote kuwa kitu kimoja na kuzika tofauti zote na amelihakikishia taifa kuwa linaviongozi wa kutosha na katiba ilio imara, hivyo kuwataka kila mmoja kuwa na matumaini na serikali iliopo kwani ametaja kuandaliwa vizuri na mtangulizi wake Rais John Magufuli pindi alivyokuwa makamu wa Rais.

Baada ya kuapishwa na kuhutubia taifa Rais Suluhu ameongoza kikao cha baraza la mawaziri katika ikulu ya Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuapishwa kwake Dar es Salaam
Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuapishwa kwake Dar es SalaamPicha: AFP/Getty Images

Katika hafla hiyo ya kuapishwa kwa rais viongozi mbalimbali wamehudhuria wakiwemo Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi,spika wa jamhuri wa muungano Job Ndugai, jaji mkuu Profesa Ibrahim Juma pamoja na mawaziri mbalimbali.

Bi Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 visiwani Zanzibar ambapo alipata elimu ya  msingi kati ya 1966 na 1972  katika shule tofauti tofati katika visiwa viwili vikubwa vinavyounda Kisiwa cha Zanzibar, ambavyo ni visiwa vya  Unguja na Pemba.

Samia Suluhu Hassani alianza safari yake ya elimu katika shule ya msingi Chawaka iliyopo kisiwani Unguja na baadae alihamia shule ya msingi Ziwani  iliyopo kisiwani Pemba kabla ya kurejea kisiwani Unguja na kumaliza elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Mahonda.