1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Zelensky: Jamii ya Kimataifa endeleeni kuishinikiza Urusi

22 Agosti 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameitaka jamii ya kimataifa kuendelea kuishinikiza Urusi kama njia pekee ya kumaliza vita huku mapigano yakiendelea kushuhudiwa dhidi ya miundombinu ya nishati na maeneo ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/4zMf4
Denmark 2025 | Rais Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aiomba jamii ya kimataifa kuendelea kusihinikiza Urusi Picha: IDA MARIE ODGAARD/AFP

Moscow imetangaza kuwa vikosi vyake vimetwaa udhibiti wa kijiji muhimu cha Aleksandro-Shultino katika eneo la Donetsk, hatua inayoonekana kuwa ya kimkakati kuelekea mji wa Konstantinovka. Wakati huohuo, Kyiv imesema vikosi vyake vimefanikiwa kurejesha sehemu kubwa ya kijiji cha Tovste katika mkoa huo na kuwatimua wanajeshi wa Urusi katika vijiji vya Zolotyi, Kolodiaz na Petrivka.

Ukraine pia imeripoti mashambulizi ya droni kwenye kiwanda cha mafuta cha Novoshakhtinsk katika mkoa wa Rostov, ghala za silaha kwenye mkoa wa Donetsk, na kituo cha mafuta katika mji wa Voronezh, yote ndani ya Urusi. 

"Leo, juhudi za kurejesha hali ya kawaida zimeendelea katika baadhi ya maeneo baada ya mashambulizi makubwa ya usiku. Urusi ilirusha zaidi ya ndege zisizo na rubani 500 — zipatazo 574 — pamoja na makombora, ikiwemo makombora ya masafa marefu, jumla ya makombora 40.” amesema Zelensky.

Urusi Unecha 2025
Moshi ukifuka kwenye kituo cha kusambaza mafuta cha Unecha nchini Urusi Picha: MAGYARBIRDS/REUTERS

Kituo cha mafuta cha Unecha chashambuliwa

Ukraine imethibitisha pia kushambulia kituo cha kusukuma mafuta cha Unecha, sehemu ya bomba la mafuta la Druzhba linalosafirisha mafuta kuelekea Hungary, Slovakia na Ujerumani. Shambulio hilo lilisababisha kusimama kwa muda kwa usafirishaji wa mafuta, hatua ambayo serikali ya Hungary imelaani kama "tishio jipya kwa usalama wa nishati.”

Kwa upande mwingine, Urusi imeendelea kulipiza kisasi kwa kushambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine, hali inayotishia upatikanaji wa gesi na mafuta ya kuendesha shughuli za kijeshi na mahitaji ya kiraia, hasa msimu wa baridi unapokaribia.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov amesisitiza kuwa uwepo wa wanajeshi wa kigeni katika ardhi ya Ukraine ni jambo lisilokubalika kwa Moscow. Amelaumu mataifa ya Magharibi kwa, kama alivyoeleza, kudhoofisha mazungumzo ya amani yaliyofanyika hivi karibuni kati ya Marekani na Urusi huko Alaska.

Na katika hatua nyingine, Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, ametoa heshima kwa wanajeshi wa nchi yake waliouawa wakipigana upande wa Urusi nchini Ukraine. Taarifa za kijasusi za Korea Kusini zinasema zaidi ya wanajeshi 600 wa Korea Kaskazini wamefariki, huku zaidi ya 10,000 wakihusishwa kupigana bega kwa bega na vikosi vya Urusi.