1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Donald Trump atatoa wito wa Umoja katika hotuba yake

5 Februari 2019

Ikulu ya Marekani imesema Rais Donald Trump atatoa wito wa matumaini na Umoja atakapotoa hotuba yake ya hali ya taifa akitumia nafasi hiyo kubadilisha hali baada ya miaka miwili ya mivutano na mataifa mengine.

https://p.dw.com/p/3ClmN
USA Krise Shutdown l Präsident Trump verkündet vorläufige Aufhebung der Haushaltssperre
Picha: Reuters/K. Lamarque

Kuna mtu yeyote atakaeyaamini maneno ya Trump katika hotuba yake ya hali ya taifa? Hilo ndilo suali linaloulizwa na wengi. Bila shaka patakuepo na shaka wakati Trump atakaposimama na kulihutubia taifa la Marekani pamoja na wabunge. 

USA Pressesprecherin Sarah Sanders
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sarah SandersPicha: Getty Images/C. Somodevilla

Wanachama wa Democrats watakaosikiliza hotuba hiyo kwa ujasiri hasa baada ya kuchukua ushindi katika uchaguzi wa nusu muhula na kukabiliana vikali na wanachama wa Republican wakati wa mkwamo wa serikali uliomalizika hivi karibuni, wanaona hakuna ushahidi mkubwa wa kuonyesha kwamba kweli Trump yuko tayari kushirikiana na wenzake.

Mkwamo wa serikali uliwaacha baadhi ya wanachama wa Republican wakikasirishwa na hatua ya Trump kusisitiza uwepo wa ukuta utakaotenganisha Marekani na Mexico kitu ambacho walikuwa tayari wameshamuonya kuwa wazo hilo halitapokelewa kwa uzuri na Wademocrat.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sarah Sanders amesema rais atazungumzia kile anachokiona kama mafanikio katika utawala wake na pia ataendelea kushinika sera ambazo zitasaidia kuuinua zaidi uchumi wa Marekani.

Rais Trump kutangaza ushindi dhidi ya wanamgambo wanaojiita dola la kiislamu IS

Katika hotuba hiyo ya hali ya taifa suala la ukuta wa mexico linatarajiwa kuzungumzwa, ambapo Trump ataendelea kuwashinikiza wademocrats wapitishe fedha za kuendeleza mpango wake wa kuujenga ukuta huo. Hatua ya Trump ya kutaka dola bilioni 5.7 za kuujenga ukuta utakaotenganisha Mexico na Marekani ilisababisha mkwamo wa serikali wa takriban siku 35.

Trump atakapokuwa analihutubia taifa lake hii leo, atakaekuwa nyuma yake ni spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi anayetokea chama cha democrats na aliyechukua nafasi hiyo baada ya chama hicho kushinda udhibiti wa bunge katika uchaguzi wa nusu muhula uliofanyika mwezi Novemna.

Kombobild Pelosi vs Trump
Spika wa baraza la wawakilishi Marekani Nancy Pelosi na rais wa Marekani Donald Trump

Bi Pelossi hadi sasa hajaonyesha dalili yoyote ya kukubaliana na Trump juu ya mradi wake wa kujenga ukuta ambao umemfanya kufikiria mara mbili kutangaza hali ya hatari ambayo Trump anasema akifanya hivyo ataweza kukusanya fedha mahala kwengine bila ruhusa ya bunge.

Kando na hilo rais huyo wa Marekani pia anatarajiwa kutangaza ushindi dhidi ya kundi la wanamgambo wanaojiita dola la kiislamu nchini Syria. Lakini maafisa wa ulinzi nchini Marekani wana wasiwasi na hofu kwamba kundi hilo huenda likawa linajipanga upya kushambulia baada ya Marekani kuondoka kabisa nchini Syria.

Hatua ya kushtukiza ya Trump kusema wanajeshi wake wanaondoka nchini Syria iliwashitua washirika wake na kusababisha waziri wa ulinzi Jim Mattis kujiuzulu pamoja na mjumbe katika muungano unaopambana dhidi ya IS Brett McGurk.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef