1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Somalia waombwa kuungana dhidi ya Al shabaab

Amina Mjahid
22 Agosti 2022

Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre amesema serikali italaumiwa kufuatia tukio la hoteli moja mjini Mogadishu kutekwa nyara na wanamgambo wa Al Shabaab aliyowaita "watoto wa Jahanamu".

https://p.dw.com/p/4FrkO
Somalia mehrere Tote bei Angriff auf Hotel Hayat in Mogadischu
Picha: Feisal Omar/REUTERS

Akizungumza baada ya kuitembelea hospitali waliko waathiriwa wa shambulio la Jana Jumapili katika Hoteli ya Hayat mjini Mogadishu, Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre amesema serikali itabebeshwa lawama na hakuna hata mtu mmoja katika serikali hiyo atakayekwepa hilo. Amesema kila aliyepuuza jukumu lake atabebeshwa dhamana.

Abdi Barre aliyechaguliwa kuwa Waziri Mkuu mwezi Juni mwaka huu, amesema njia ni mbili tu aidha al-shabaab waendelee kuwepo kuishi duniani au Somalia ipambane nao kwa nia ya kuwasambatisha kabisa. 

Kando na hilo Waziri Mkuu huyo pia amewatolea wito  raia wa Somalia kuungana katika mapambano dhidi ya Kundi hilo la Al shabaab lililo na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda. Al Shabaab wamekuwa wakiendeleza mashambulizi ya umwagikaji damu katika taifa hilo la Pembe ya Afrika kwa zaidi ya miaka 15.

Huku hayo yakiarifiwa, Waziri wa Afya wa Somalia Ali Haji Adan amesema Idadi ya watu waliouwawa katika shambulio hilo imepanda na kufikia 21, lakini msemaji wa kundi la Al shabaab Abdiaziz Abu-Musab ameweka idadi ya vifo kuwa 40. 

Wachambuzi wasema shambulio ni jibu kwamba Alshabaab bado wananguvu

Somalia Mogadishu | Al-Shabaab Kämpfer während Militärübung
Baadhi ya wanamgambo wa kundi la Al shabaabPicha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Shambulio hilo lililochukua zaidi ya saa 30 lililohusisha ufayatulianaji wa risasi na mabomu lilisababiha baadhi ya sehemu ya hoteli ya Hayat kuporomoka na watu wengi wanahofiwa kukwama chini ya vifusi vya jengo hilo. Tayari wafanyakazi wa huduma za dharura na wataalamu wa kutegua mabomu wapo katika eneo hilo kuanzia jana wakitafuta mabomu yatakayokuwa yametegwa katika eneo hilo.

Hoteli ya Hayat ni eneo maarufu la maafisa wa serikali kukutana na watu wengi walijeruhiwa wakati mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliporusha bomu na kuzua tafrani kabla ya yeye na wenzake kuingia katika hoteli hiyo na kuiteka kwa zaidi ya saa 30.

Washirika wa Somalia ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya, Uturuki na Umoja wa Mataifa wamelaani shambulio hilo. Ujumbe wa mpito wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, maarufu kama ATMIS, uliochukua nafasi ya kikosi cha AMISOM na kuwa na jukumu la kuisaidia serikali ya Somalia kuchukua nafasi yake kikamilifu  ifikapo mwaka 2024 pia imelaani shambulio hilo.

Samira Gaid, Mkurugenzi wa taasisi ya Hiraal iliyoko Mogadishu inayoshughulikia masuala ya usalama amesema shambulio hili ni ujumbe kwa serikali mpya pamoja na washirika wake  kwamba bado Al-Shabaab wapo na wananguvu.

Chanzo: AFP