Raia 5 wa Msumbiji wauawa katika mashambulizi Afrika Kusini
2 Juni 2026
Taarifa hiyo inaeleza kuwa takriban Wamsumbiji 800 walikumbwa na vurugu katika mji wa Mossel Bay, ambako maandamano dhidi ya wahamiaji wasiokuwa na vibali yameongezeka.
Takriban watu 300 walirejea Msumbiji, huku zaidi ya 500 wakihifadhiwa eneo salama wakati mchakato wa kuwarejesha ukiendelea.
Maafisa wa Afrika Kusiniwanasema wanachunguza vifo hivyo, wakati viongozi wa eneo hilo wakielezea wasiwasi kuhusu mauaji, uchomaji nyumba na watu kukimbia makaazi yao.
Serikali ya Msumbiji imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na mamlaka za Afrika Kusini ili kuhakikisha usalama wa raia wake na kufanikisha kurejea kwao salama nyumbani.
Aidha, imewataka wananchi wake walioko Afrika Kusini kuwa waangalifu na kufuata maelekezo ya usalama yanayotolewa na mamlaka husika.
Kwa upande wao, viongozi wa mitaa katika eneo la Mossel Bay wameelezea hofu kuwa hali hiyo inaweza kuendelea kuzorota iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kudhibiti ghasia hizo.
Mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni yamekuwa yakijirudia nchini Afrika Kusini kwa miaka kadhaa, hasa yakilenga wahamiaji kutoka mataifa jirani wanaotuhumiwa kuchukua ajira na rasilimali.