1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Dibobe: Kutoka maonesho hadi mwanaharakati dhidi ya ukoloni

27 Desemba 2023

Quane Martin Dibobe alipelekwa Ujerumani kuongeza hamasa kwa ukoloni wa Ujerumani, lakini alikuja kuwa mwanaharakati wa haki za binaadamu aliyepinga unyonyaji wa Ujerumani kwa makoloni yake.

https://p.dw.com/p/4adiW
Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.
Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Quane Martin Dibobe alikuwa nani?


Dibobe alizaliwa karibu na mji wa Douala nchini Kameruni mwaka 1876, ambako baba yake alikuwa na nafasi kwenye siasa.

Alipata elimu yake kwenye skuli ya misheni nchini Kameruni, ambalo alijifunza kusoma na kuandika kwa Kijerumani.

Soma zaidi: Togo "Koloni la Mfano"

Aliwasili nchini Ujerumani katikati ya miaka ya 1890 kushiriki Maonesho Makubwa ya Viwanda ya Berlin.


Yapi yalikuwa maonesho ya kwanza ya ukoloni wa Ujerumani mwaka 1896?


Maoenesho hayo yalikuwa na dhamira ya kuonesha kwamba Ujerumani ilikuwa "nchi yenye fursa zisizo kifani."

Propaganda kubwa ilikuwa ikiendeshwa kuwashawishi Wajerumani kwamba ilikuwa ni haki kwa Ujerumani kuwa na makoloni.

Propaganda hiyo ilijumuisha maonesho ya kiethnolojia ya "maisha ya kila siku kwenye makoloni."

Soma zaidi: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"

Hivi leo, tungeliyaita maonesho hayo kuwa ni zizi la wanaadamu.

Dibobe alikuwa mmoja kati ya zaidi ya Waafrika 100 waliowasili Berlin - wengine wakiwa wamechukuliwa kwa nguvu, wengine wakidanganywa kwa ahadi za malipo.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani

Walikuja wakitokea kwenye makoloni ya Kijerumani ya Namibia, Togo, Tanzania na Kameruni - miongoni mwao wakiwa watu wa jamii za Ovaherero, Nama na Maasai.

Quanne Dibobe akifahamika kama "Nambari 76." Kiuhalisia, yeye na wenzake hawakufanana na "wenyeji washenzi" waliokuwa wakioneshwa kwenye vijiji vya kubuni.

Wajerumani wapatao milioni saba walifurika kwenye maonesho hayo kwa zaidi ya miezi sita kumuona Dibobe na wenzake wakati wakilazimishwa kuigiza maisha ya kubuni - kupika, kucheza, kuwinda - kwenye kijiji cha uongo cha Afrika.

Dibobe na wengine wengi walilazimishwa kufanyiwa uchunguzi wa kidhalilifu uliofanywa na wanafunzi wa sayansi ya ubaguzi wa rangi wa Ujerumani - kwa lengo la kuthibitisha sayansi ya uongo ya yojeniksia.

Dibobe alifanya nini baada ya maonesho hayo?

Dibobea alibakia mjini Berlin, jambo ambalo halikuwa la ajabu sana. Waafrika wachache walikuwa mara nyingi wanakubalika kwenye miji mikubwa, ambako wangeliweza kupata kazi au mafunzo.

Kwanza Dibobe alifanya kazi za mikono kabla ya kujiunga na kampuni ya reli ya Berlin.

Soma zaidi: Uporaji wa ardhi: Kuzaliwa kwa Himaya ya Ukoloni wa Ujerumani

Alimuoa binti wa mpangishaji wake wa nyumba baada ya mmishionari aliyembatiza Dibobe nchini Kameruni kuthibitisha utambulisho wake.

Kufikia mwaka 1902, Dibobe alishakuwa dereva wa treni mjini Berlin - kazi ya heshima kubwa wakati huo - na akawa mtu mashuhuri.

Kivuli cha ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Kwanza

Baadaye alikuja kuandika: "Kupitia juhudi kubwa na tabia isiyotilika shaka, nilipata nafasi ya kuaminiwa."

Je, Dibobe aliwahi kurudi tena Kameruni?

Serikali ya kikoloni ilimrudisha Dibobe nchini Kameruni mwaka 1907 kuwa mshauri kwenye ujenzi wa njia ya reli.

Njia hiyo iliyojengwa na Wajerumani ipo hadi leo nchini Kameruni, na baadhi ya wanahistoria wanazungumzia hamu ya watu kwa zama za Mjerumani, hasa zinapolinganishwa na matendo ya kinyonyaji ya Ufaransa na Uingereza, zilizoyatwaa makoloni ya Ujerumani baada ya mwaka 1919.

Soma zaidi: Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni

Lakini Dibobe alishitushwa sana na vipigo, utwaaji wa mali za wenyeji, ubaguzi wa rangi na matendo machafu waliyotendewa Wakameruni na kampuni za Kijerumani.

Hadhi ya raia wa makoloni ya Kijerumani ilikuwa vipi?

Nchini Ujerumani, Dibobe alishiriki kwenye migomo ya wafanyakazi, aliunga mkono chama cha Social Democrat na alikuwa mwanachama wa Baraza la Haki za Binaadamu lililoundwa mwaka 1914.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Pili

Kadiri Waafrika wengi walivyowasili kwenye miji kama vile Berlin, Hamburg na Bremen, Dibobe na wengine wengi waliobakia Ujerumani walijikuta wakiwa hawana uraia wa nchi yoyote.

Soma zaidi: Mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20

Serikali ya Ujerumani haikuwa na dhamira yoyote ya kuwapa raia kutoka makoloni yake haki sawa na raia wa Kijerumani kwani hilo lingelimaanisha sheria inapaswa kutekelezwa kwa usawa kwenye makoloni yote.

Kwa hivyo, katikati ya mwaka 1919, kwa niaba ya Waafrika wanaoishi kwenye makoloni ya Ujerumani, Dibobe na Wajerumani 17 wenye asili ya Afrika waliiandikia serikali kudai uwakilishi, haki sawa na kukomeshwa kwa ufanyishaji kazi kwa lazima, miongoni mwa nukta 32  walizoziandika, na wakati huo huo wakatangaza utiifu wao kwa Jamhuuri ya Waimer ya Ujerumani.
 

Kipi kilitokea kwa andiko hilo la Dibobe?


Kwa kuwa Ujerumani ililazimika kuyakabidhi makoloni yake kwa mataifa mengine ya Ulaya kwa mujibu wa Mkataba wa Versailles, matakwa ya andiko hilo kamwe hayakutambuliwa.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Utwaaji wa ardhi

Dibobe alipoteza kazi yake ya reli.

Alijaribu kurudi nchini Ujerumani mwaka 1922, lakini watawala wa kikoloni wa Ufaransa walimkatalia kuingia kwa sababu waliamini angelisababisha machafuko.

Soma zaidi: Maonyesho kuhusu wajerumani weusi mjini Cologne

Badala yake, akiwa na umri wa miaka 45, Dibobe alielekea Liberia na hakuonekana tena. Inaaminika kuwa alikufia huko.

Matokeo yake, Dibobe hafahamiki sana nchini Kameruni, ingawa sehemu kubwa ya kumbukumbu zake inatambuliwa nchini Ujerumani.

Lakini karne nzima baadaye, andiko lake linachukuliwa kama mojawapo ya nyaraka muhimu kabisa za wahamiaji wa Kiafrika wa karne ya 21.

Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.