1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Putin asema Zelenskiy hana uhalali baada ya muda wake kuisha

25 Mei 2024

Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema jana kuwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy hana tena uhalali baada ya kumalizika kwa muhula wake bila kufanyika uchaguzi mpya.

https://p.dw.com/p/4gGri
Rais Putin akiwa na mshirika wake wa Belarus, Alexander Lukashenko.
Rais Putin akiwa na mshirika wake wa Belarus, Alexander Lukashenko.Picha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Rais Putin amesema suala hilo linaweza kuibua vikwazo vya kisheria iwapo Urusi na Ukraine zitaamua kufanya mazungumzo ya amani.

Wakati Ukraine ikitawaliwa kwa sheria ya kijeshi katika mwaka wa tatu wa vita vya uvamizi wa Urusi, Zelenskiy hajaitisha uchaguzi licha ya muhula wake kumalizika wiki hii - jambo ambalo yeye na washirika wa Ukraine wanalichukulia kuwa uamuzi sahihi katika wakati wa vita.

Shirika la habari la Reuters limeripoti jana likinukuu vyanzo vinne vya Urusi, kuwa Putin yuko tayari kusitisha vita nchini Ukranine kwa mapatano yanayotambua misitari ya sasa ya uwanja wa vita, lakini pia yuko tayari kuendeleza mapambano ikiwa Kyiv na washirika wake wa magharibi hawatajibu.

Kwenye mkutano wa habari uliotangazwa kwenye televisheni wakati wa ziara nchini Belarus, Putin alisema hadhi ya Zelenskiy ilikuwa na matatizo.