1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Presseschau: Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
5 Oktoba 2017

Maoni ya wahariri wa magazeti leo yametuama katika mauaji yaliyotokea huko Las Vegas, wanatoa maoni juu ya mgogoro wa jimbo la Catalonia na pia wameangazia mkutano mkuu wa chama cha kihafidhina cha nchini Uingereza. 

https://p.dw.com/p/2lFS3
Spanien Katalonien Unabhängigkeits-Referendum - Fernsehansprache von Rajoy
Picha: Getty Images/AFP/J. Soriano

Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema ikiwa mawasiliano hayatadumishwa ndani ya Uhispania jimbo mojawapo tajiri katikati mwa barani Ulaya litakuwamo katika hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mhariri anatilia maanani mfululizo wa matukio ya kusikitisha ukiwa unaelendelea, muflisi wa Ugiriki,ushindi wa makundi yenye  itikadi kali za mrengo wa kulia, mgogoro wa wakimbizi na kura ya maoni juu ya Uingereza kujindoa Umoja wa Ulaya (Brexit).

Naye mhariri wa Die Volksstimme ameandika pia juu ya mgogoro wa Catalonia anasema kiogozi wa  jimbo la Catalonia, Carles Puigdemont ameitisha  kura ya maoni mapema mno na  hivyo  kusababisha  uchokozi wa hali ya juu kabisa.  Kwa bahati mbaya Waziri Mkuu Mariano Rajoy amefanya  pupa  na  ameingia katika mtego kwa kuwapelaka polisi waliotembeza virungu kwa waandamanaji.  Katikati ya Ulaya katika karne hii ya 21, kushindwa kwa viongozi wachache kuchukua hatua sahihi, kunaweza kusababisha maafa  makubwa.

Nini kitafanyike baada ya maafa ya Las Vegas kutokea

Gazeti la Aachener Zeitung linasema ikiiwa wendawazimu huo hautokomeshwa kwa sheria kali, hakuna kitakachobadilika nchini Marekani. Lakini uwezekano wa kubadilisha sheria ya umiliki wa bunduki ni nunge kabisa kwenye bunge la Marekani linalodhibitiwa na wajumbe wa chama cha Republican. Na kutokana na uwepo wa rais Trump anaetaka kuwaruhusu watu kuwa na silaha kote nchini Marekani ina maana uwezekano huo kwa sasa haupo.

Kuhusu mkutano mkuu wa chama cha kihafidhina cha Uingereza

Gazeti la Stuttgarter Zeitung juu ya mkutano mkuu wa chama cha kihafidhina nchini  Uingereza. Mhariri wa gazeti hilo ameandika kwamba mkutano huo uliofungwa kwa hotuba  ya Waziri Mkuu Theresa May ulikuwa wa maafa. Mhariri wa gazeti hilo la Stuttgarter Zeitung anaeleza kwamba kwanza waziri wake wa mambo ya nje Boris Johnson kwa ujeuri alimpa changamoto kwa kuupinga mkakati wake juu Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya.  Bibi May pia alipaswa kwa muda wa siku tatu kusikiliza jinsi mawaziri wake pamoja wajumbe wengine walivyokuwa wanalumbana juu ya nchi yao kujiondoa Umoja wa Ulaya (Brexit) kana kwamba kadhia hizo hazikutosha, sauti yake ilikauka wakati alipoihitaji zaidi kuwapa sauti hiyo wale waliosahauliwa katika jamii ya Waingereza.      

Mwandishi: Zainab Aziz/ Deutschen Zeitungen

Mhariri: Iddi Ssessanga