1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiLebanon

Papa Leo XIV awasili Lebanon na ujumbe wa amani

Saleh Mwanamilongo
30 Novemba 2025

Kiongozi wa Kanisa katoliki duniani, Papa Leo wa XIV amewasili nchini Lebanon leo Jumapili kwa ziara ya siku mbili, ambapo anatarajiwa kutoa ujumbe wa amani.

https://p.dw.com/p/54W4f
Lebanon, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Wakristo Mashariki ya Kati, imeathirika na vita vya Gaza
Lebanon, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Wakristo Mashariki ya Kati, imeathirika na vita vya GazaPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa Kanisa katoliki duniani, Papa Leo wa XIV amewasili nchini Lebanon Jumapili kwa ziara ya siku mbili, ambapo anatarajiwa kutoa ujumbe wa amani. Kwa mujibu wa mwandishi wa AFP aliyekuwa ndani ya ndege ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, amesema Papa Leo ametua Beirut akitokea Uturuki. Papa atakutana na Rais Joseph Aoun, kiongozi pekee Mkristo katika ulimwengu wa Kiarabu, na baadaye atatoa hotuba kwa viongozi na wanadiplomasia katika ikulu ya rais.

Papa Leo pia anatarajiwa kutembelea eneo kulipotokea mlipuko mkubwa kwenye bandari ya Beirut. Mlipuko huo uliotokea miaka mitano iliyopita uliwaua watu 220.

Anapanga kukutana na waathirika na vijana, kwa lengo la kuwafaraji na kuhimiza mshikamano. Ziara hii inakuja wakati hofu ya kurejea kwa vita na Israel bado ipo, huku Vatican ikisisitiza Lebanon isalie kuwa ngome ya Wakristo katika eneo lenye misukosuko.