Ngudjolo Chui atakaswa na Mahakama kuu ya Kimataifa | Magazetini | DW | 21.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ngudjolo Chui atakaswa na Mahakama kuu ya Kimataifa

Mada kadhaa zimehodhi kurasa za Afrika katika magazeti ya Ujerumani ,ikiwa ni pamoja na uamuzi wa mahakama kuu ya kimataifa mjini The Hague na kutakiwa wakimbizi wa kisomali warejee kambini nchini Kenya

Mathieu Ngudjolo Chui katika ukumbi wa mahakama kuu ya kimataifa mjini The Hague

Mathieu Ngudjolo Chui katika ukumbi wa mahakama kuu ya kimataifa mjini The Hague

Tuanzie The Hague ambako mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, imemtakasa wiki hii aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo wa Ituri - FRPI, Mathieu Ngudjolo Chui, na dhana za kuhusika na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Haikuwezekana kupata ushahidi bayana wa makosa ya bwana huyo mwenye umri wa miaka 42 limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine likiinukuu hoja iliyotolewa na mahakama kuu hiyo ya kimataifa. Madai hayo yanatokana na mashambulio ya Februari 2003 katika kijiji cha Bogoro ambapo watu wasiopungua 200 waliuliwa na takriban wakaazi wote wa kike wa kijiji hicho kubakwa. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limekumbusha kesi nyengine kuhusu kisa hicho inayoendelea mjini The Hague dhidi ya Germain Katanga ambaye sawa na Ngudjolo Chui, anashitakiwa kuhusika na mashambulio katika kijiji cha Bogoro, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mbali na Frankfurter Allgemeine, gazeti la die Tageszeitung pia liliichambua kesi dhidi ya viongozi hao wawili wa wanamgambo wa Ituri, na kusema haijulikani bado hukumu dhidi ya Germain Katanga itapitishwa lini. Die Tageszeitung linahisi kuna suala la kuuliza la kisiasa linalojitokeza ikizingatiwa kwamba miezi tisa tu iliyopita mahakama hii hii ya kimataifa ya mjini The Hague imemkuta na hatia na kumhukumu miaka 14 jela, kiongozi mwengine mkuu wa wanamgambo wa Ituri, Thomas Lubanga, kwa kuwaandikisha jeshini watoto. Watu katika eneo la Ituri wanauwekea swali la kuuliza uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague kwa kumhukumu kiongozi wa wanamgambo wa kabila la Hema na kumtakasa yule wa kabila la Lendu.

Flüchtlinge Dadaab Somalia Kenia Hungersnot Frauen Kinder

Kambi ya wakimbizi wa kisomali ya Dadaab nchini Kenya

Uamuzi wa serikali ya Kenya kuwataka wakimbizi wa kisomalia warejee kambini badala ya kukaa mijini ni kisa kilichochambuliwa pia na magazeti ya Ujerumani wiki hii. Lilikuwa gazeti la Süddeutsche Zeitung lililozungumzia kadhia hiyo, baada ya kuzungumzia sababu zilizowafanya wasomali hao wakimbilie Kenya. Süddeutsche Zeitung linayataja mashambulio kadhaa ya maguruneti yanayoutikisa mji mkuu Nairobi kuwa sababu ya uamuzi huo wa serikali ya Kenya. Watu zaidi ya 13 wamepoteza maisha yao na wengi wengine kujeruhiwa kutokana na mashambulio hayo ambayo hadi wakati huu haijulikani yamefanywa na nani. Inaaminiwa wanamgambo wa itikadi kali Al Shabab pengine wako nyuma ya mashambulio hayo. Süddeutsche Zeitung limewanukuu baadhi ya wakimbizi wa kisomali wanaoishi mjini Nairobi wakisema wameshaanza kujikwamua kimaisha, wakirejea kambini, maisha yao yatavurugika."

Lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine lililozungumzia kuhusu mkutano mkuu wa 53 wa chama tawala cha African National Congress, ANC, uliomuidhinisha Jacob Zuma kuendelea kukiongoza chama hicho. Kwamba atashinda ilikuwa dhahiri, kisichojulikana ni kama Kgalema Montlanthe ataendelea kuwa msaidizi wa rais baada ya kushindwa katika uchaguzi huo na malumbano ya kabla ya uchaguzi.

Deutschland Terror Bonn Behörden suchen nach Bombenfund weiter nach Verdächtigen

Kituo kikuu cha safari za reli mjini Bonn ambako magaidi wa itikladi kali walitega mkoba uliosheheni miripuko.

Na hatimaye lilikuwa gazeti la Kölner Stadt Anzeiger lililoichambua hali namna ilivyo nchini Mali pamoja na juhudi za Ulaya kuwasaidia wanajeshi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi kukabiliana na wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu wanaolidhibiti eneo la kaskazini la nchi hiyo. Kölner Stadt Anzeiger limejaribu kujibu hoja za wale wanaojiuliza kwa nini nchi za Ulaya zisaidie katika nchi hiyo iliyoko mbali kabisa kijiografia, kitamaduni na hata kisiasa. Jibu la suala hilo linaandika gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linapatikana katika njama ya shambulio katika kituo kikuu cha safari za reli mjini Bonn na Cologne hapo awali. Mifuko iliyosheheni miripuko iliyogunduliwa katika vituo hivyo imewekwa na watu wanaosemekana kuwa na mafungamano na makundi ya itikadi kali ya dini ya kiislamu. Al Qaida wanaiangalia Afrika kuwa ni daraja ya kuingia Ulaya, linamaliza kuandika gazeti hilo la mjini Cologne.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/ALL PRESSE

Mhariri: Josephat Charo