1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nagelsmann ashinda mechi ya kwanza na timu ya taifa

16 Oktoba 2023

Julian Nagelsmann ameshinda mechi yake ya kwanza kama kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani kwa ushindi wa 3-1 ugenini katika mechi ya kirafiki dhidi ya Marekani siku ya Jumapili (Oktoba 15).

https://p.dw.com/p/4XbAQ
Fussball Freundschaftsspiel | Deutschland - USA
Kocha mpya wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, katika mechi ya kirafiki dhidi ya Marekani.Picha: Federico Gambarini/dpa/picture alliance

Ushindi huo rahisi ulikuwa mafanikio makubwa kwa Nagelsmann, ikizingatiwa kwamba mtangulizi wake,Hansi Flick, alishindwa kushinda mchezo wowote kati ya mechi tano za mwisho.

Hata hivyo, mabadiliko ya ukufunzi hayakubadilisha udhaifu uliopo katika safu ya ulinzi ya timu ya taifa ya Ujerumani.

Soma pia: Nagelsmann kocha mpya wa Ujerumani kuelekea Euro 24

Ujerumani imekuwa na mapungufu katika safu ya beki wa kulia tangu alipostaafu Philipp Lahm, na imeendelea na utaratibu wa kuwapanga mabeki wa kati kwenye nafasi hiyo.

Dhidi ya Marekani, Nagelsmann aliamua kumweka Jonathan Tah wa Bayer Leverkusen.

Kocha wa timu ya taifa ya Marekani, Gregg Berhalter, alisema timu yake ilikuwa inahitaji kujifunza wakati wakijiandaa kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026.

Fussball WM Katar l  Niederlande - USA l Gregg Berhalter USA, Trainer
Picha: Frank Hoermann/SVEN SIMON/picture alliance

"Tulichojifunza ni kasi ambayo timu hizi za juu zinaweza kucheza, jinsi wanavyocheza katika nafasi ngumu. Ilikuwa muhimu kujifunza. Na kisha nadhani pia kwa sisi kuelewa kwamba tunaweza pia kuumiza timu kama hiyo. Na inapaswa kutupa imani kidogo. Na tunapojiandaa  kuelekea 2026, kwa njia hii, ni kujifunza wakati huu na kuelewa kwamba tunahitaji kuwa makini katika kila dakika ya mchezo ili kupata nafasi." Alisema kocha huyo wa Marekani.

Nagelsmann hajaridhika

Hata hivyo, licha ya kupata ushindi katika mechi yake ya kwanza, Nagelsmann, alisema bado kuna udhaifu,

"Tutajaribu kucheza kwa kiwango cha juu katika siku zijazo. Tunahitaji suluhu katika kujilinda katika nusu yetu lakini pia kubana zaidi wakati tunaposhambulia. Kwa hivyo tutajaribu kufanyia kazi shinikizo letu la juu, kujinda na pia kusonga mbele. Tutajitahidi kuendelea hivi hivi,  sio kila kitu leo kilikuwa shwari ila ni vizuri kwa sababu napenda kufanya kazi. Kwa hiyo tufanye kazi." Alisema kocha huyo wa Ujerumani.

Ujerumani inatarajia kuchuana na Mexico katika mechi nyengine ya kirafiki Jumatano wiki hii, kuendelea kujiandaa kwa michuano ya ubingwa wa Ulaya itakayokuwa mwenyeji wake.

Soma pia:Ni mapema kujua mshindi wa ligi ya mabingwa Ulaya 

Kufikia sasa, tayari Ufaransa, Ubelgiji, Ureno, Uhispania, Uturuki na Scotland zimejihakikishia nafasi katika michuano ya kuwania Ubingwa wa Ulaya 2024.