1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi waongezeka kuhusu mzozo wa Kosovo na Serbia

Saumu Mwasimba
1 Juni 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken azitaka pande zote mbili zichukue hatua ya haraka kupunguza mvutano

https://p.dw.com/p/4S4vN
Kosovo | KFOR Friedensmission
Picha: Erkin Keci/AA/picture alliance

Mzozo kati  ya Kosovo na Serbia unazidi kuitia wasiwasi jumuiya ya Kimataifa. Hii leo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amezitaka pande zote mbili zichukue hatua ya haraka kupunguza mvutano huku akitahadharisha kwamba hali ya hivi sasa inakwamisha michakato ya kuzijumuisha nchi hizo katika ushirikiano wa nchi za Ulaya na zile za ukanda wa bahari ya Atlantiki.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken hii leo baada ya kuzungumza na mawaziri wenzake wa Jumuiya ya kujihami ya NATO huko Oslo alisema washirika wengi wa jumuiya hiyo wameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu mvutano unaoendelea kaskazini mwa Kosovo baada ya mameya kutoka jamii ya Walbania kutwaa udhibiti wa ofisi za maeneo chungunzima ya Kaskazini mwa Kosovo yanayokaliwa zaidi na  jamii ya Waserbia.Na akatowa mwito wa kusitishwa mara moja mvutano huo.

Kosovo | KFOR Friedensmission
Picha: Erkin Keci/AA/picture alliance

"Tunazitaka serikali za Kosovo na Serbia kuchukua hatua za haraka kusitisha mvutano  na kuanzisha upya juhudi za utekelezaji makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Ulaya. Tunaunga mkono mchakato wa kuzijumuisha pande zote mbili kwenye ushirikiano wa Ulaya na kanda ya bahari ya Atlantiki lakini hali ya mvutano ya hivi sasa inazuia kuliko kusaidia juhudi za kwenda kwenye mwelekeo huo.''

Mgogoro wa sasa ulijitokeza  baada ya uchaguzi wa manispaa mnamo mwezi Aprili ambao hata hivyo jamii ya Waserbia waliususia na hatua yao hiyo iliwafanya Wakosovo wa jamii ya Waalbania kuyadhibiti mabaraza yote ya miji licha idadi ya wapiga kura waliojitokeza kuwa chini ya asilimia 3.5.

Kosovo | KFOR Friedensmission
Picha: Bojan Slavkovic/AP Photo/picture alliance

Hii leo alhamisi Waserbia walikusanyika kwa mara nyingine katika mji ambao ni kitovu cha mvutano wa Zvecan ambako yalizuka machafuko mwanzoni kabisa mwa wiki hii na wanajeshi wanaoongozwa na Jumuiya ya NATO katika jimbo la Kosovo, wakati shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa zikiongezeka kuutaka utawala wa mjini Pristina kusitisha mvutano huu.

Katika mji huo wa Zvecan kiasi waandamanaji 70 walikusanyika nje ya ofisi kuu ya manispaa ya mji iliyozunguushiwa waya wa senyenge na kuzunguukwa na wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani kinachoongozwa na NATO cha KFOR wakiwa wamejihami kikamilifu kukabiliana na fujo.

Mnamo siku ya Jumatatu zilizuka pia vurugu, mamia ya watu walikusanyika upande wa Kusini kwenye idadi kubwa ya jamii ya Walbania ambako ndiko kwenye mji uliogawika wa Mitrovica lakini maandamano hayo yalivunjika baada ya nusu saa.Watu hao walionekana wakipeperusha bendera za Albania huku wakiimba kwamba Mitrovica hauwezi kuwagawanywa.  Kimsingi jamii ya Waserbia inataka kuondolewa kwa vikosi maalum vya askari  kutoka Kosovo pamoja na mameya wenye asili ya  Albania ambao inasema sio wawakilishi wao.

Antony Blinken | US-Außenminister
Picha: Sergei Grits/AP Photo/picture alliance

Marekani ambayo ni mshirika wa kihistoria wa Kosovo na ambayo ndiyo hasa iliyopambania uhuru wa jimbo la Kosovo kutoka Serbia,imeikosoa serikali hiyo ya Pristina kwa kuzidisha mgogoro bila sababu kwa kuwaingiza kimabavu mameya Wakialbania katika maeneo ya jamii za Waserbia ndani ya  Kosovo. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nae pia ameikosoa serikali ya Kosovo akiitwika lawama kwamba ndiyo inayowajibika kwa hali iliyopo sasa.

Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wanatarajiwa kukutana na rais wa Kosovo Vjosa Osmani na mwenzake wa Serbia Aleksandar Vucic pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Moldova. Kosovo ilijikomboa dhidi ya Serbia na kujitangazia uhuru wake mwaka 2008 ingawa utawala wa Belgrade pamoja na washirika wake,China na Urusi bado hauitambui hatua hiyo ya Kosovo,jambo ambalo linaizuia Kosovo kupata kiti kwenye Umoja wa Mataifa.

Kosovo yenyewe idadi kubwa ya wakaazi wake ni jamii ya Waalbania lakini jamii ya Waserbia nao ni asili mia 6 na kwa kiasi kikubwa imebakia kuwa watiifu kwa serikali ya Serbia mjini Belgrade na hasa wale walioko upande wa Kaskazini ambako ndio wenye idadi kubwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso Ibrahim Traore akizungumza na waandishi wa habari mjini Ouagadougou, Burkina Faso Oktoba 2, 2022
Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW
Nenda ukurasa wa mwanzo