Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku tano | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 02.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku tano

Takwimu zilizotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusu usalama wa waandishi wa habari zinaonyesha kwamba kila baada ya siku tano mwandishi mmoja huuawa duniani kote.

Takwimu hizo zinakuja sambamba na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili wa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNESCO, karibu wanahabari 827 waliuawa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita,115 kati yao wakiuawa mwaka jana pekee na kuufanya mwaka 2015 kushikilia nafasi  ya pili kwa mauaji ya waandishi wa habari wengi katika muongo mmoja uliopita.

UNESCO inasema nchi kadhaa zimeonyesha dhamira ya kukomesha mauaji ya waandishi licha ya kwamba ni kesi chache zinazohusu vifo vya waandishi ambazo zimeshughulikuwa au kupatiwa ufumbuzi.

Maandamano ya waandishi wa habari ya mjini Cairo, Misri Mei 3

Maandamano ya waandishi wa habari ya mjini Cairo, Misri Mei 3

Ripoti ya shirika hilo kwa mwaka huu ilijikita zaidi katika usalama wa waandishi wa habari dhidi ya mauaji katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na imeonyesha kwamba haikuangalia madhila mengine yanayowakumba waandishi ikiwemo utekaji nyara, kukamatwa kiholela, mateso, vitisho na unyanyasaji.

Mataifa ya uarabuni ni hatari zaidi

Kati ya waandishi 213 waliouawa katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015, waandishi 78 waliuawa katika mataifa ya kiarabu pekee kwa mujibu wa takwimu za UNESCO na kuufanya ukanda huo kuwa eneo hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao, sababu kubwa ikiwa ni vita inayoendelea katika mataifa ya Syria, Yemen, Iraq na Libya.

Katika kipindi hicho hicho jumla ya waandishi 58 waliualiwa Amerika ya Kusini na ukanda wa Karibeani, 34 waliuawa Asia, barani Afrika waandishi waliouawa ni 27 na 12 waliuawa Ulaya ya kati na mashariki.

Nusu ya waandishi wa habari za mitandaoni waliouawa katika miaka miwili iliyopita ni waandishi wa blogs na wale wa tovuti waliokuwa wakiripoti juu ya vita ya Syria.

Katika ukanda wa Afrika mashariki Sudan Kusini imeonekana kuwa na idadi kubwa ya mauaji ya waandishi ambapo jumla ya waliouwa ilifikia tisa ikifuatiwa na Uganda waandishi wa habari 4 huku nchi zilizosalia wakiripotiwa kuuliwa mwandishi mmoja hadi wawili.

Türkei | Recep Erdogan bei der Eröffnung der High Speed Train Station in Ankara (picture-alliance/abaca)

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ametajwa kuwa adui wa uhuru wa habari

Waandishi wa habari wanawake wameonekana kulengwa zaidi katika mauaji hayo tofauti na takwimu za miaka iliyopita. Waathirika wakubwa wa mauaji hayo ni waandishi wa habari wa ndani ukilinganisha na wale wa kigeni. Kwa takwimu hizo UNESCO inasema uhuru wa vyombo vya habari bado umegubikwa na giza na kwamba kasi ndogo ya kushughulikia kesi za mauaji hayo na ongezeko la ukatili wa uhalifu dhidi ya waandishi kunaibua mijadala ya kitaifa pamoja na kulenga kuvinyamazisha vyombo vya habari.UNESCO inasema usalama wa waandishi wa habari utawezekana ikiwa masuala matatu ya kuzuia, kuwalinda na kuwashitaki wanaohusika yatashughulikiwa. 

Adui wa uhuru wa habari

Na katika tathmini ya maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wasio kuwa na mipaka wameorodhesha jumla ya wakuu wa nchi 35 na serikali, makundi yenye itikadi kali na idara za ujasusi ambapo kwa mara ya kwanza rais wa Uturuki Tayyip Erdogan yupo katika orodha hiyo. Tathmini hiyo inasema Erdogan anadhibiti kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari vya kitaifa na kuongeza kwamba jumla ya wanahabari 130 wamefungwa huku vyombo vya habari 140 navyo vikifungiwa nchini Uturuki.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpae,http://en.unesco.org/dg-report

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com