1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Museveni aadhimisha miaka 40 ya utawala wake Uganda

26 Januari 2026

Sherehe za kuadhimisha miongo minne ya uongozi wa Rais Museveni tangu achukue madaraka 1986, yageuka jukwaa la lawama za kisiasa.

https://p.dw.com/p/57UBj
Uganda Kampala 2026 | Rais Yoweri Museveni alipomaliza kampeni yake kabla ya uchaguzi wa bunge
Museveni awaita wapinzani kuwa magaidi na wameendelea kuwatishia wafuasi wakePicha: AFP

Matamshi ya Rais Yoweri Museveni kuwataja wapinzani wake kuwa magaidi, aliyoyatoa wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya utawala wake, yameibua mjadala mpana wa kisiasa na yamepokelewa kwa hisia na mitazamo tofauti ndani na nje ya Uganda.

Sherehe hizo zililenga kuadhimisha miongo minne ya uongozi wa Rais Museveni tangu achukue madaraka mwaka 1986 kupitia vuguvugu lake la NRM, hata hivyo, maadhimisho hayo yaligeuka kuwa jukwaa la lawama za kisiasa.

Wanaharakati wa utawala wa kidemokrasia wamesema matamshi hayo yanaashiria hali ya wasiwasi na mashaka miongoni mwa viongozi wa upinzani, hasa katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi.

Sherehe za maadhimisho zilifanyika siku chache baada ya uchaguzi mkuu ambapo Rais Museveni alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 71 ya kura, huku mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi akipata asilimia 24.

Museveni: Vitisho vilisababisha wapiga kura kutojitokeza kwa wingi

Katika hotuba yake, Rais Museveni ameeleza kutoridhishwa kwake na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi mkuu, akidai kuwa zaidi ya wafuasi wake milioni sita hawakushiriki uchaguzi kutokana na vitisho na matamshi aliyoyataja kuwa ya kigaidi kutoka kwa upinzani. Museveni alishangaa ni kwa nini vyombo vya usalama havikuwachukulia watu waliotoa matamshi hayo hatua stahiki.

"Wapinzani ni magaidi na wameendelea kuwatishia wafuasi wangu. Ndiyo maana wengi waliogopa kushiriki katika uchaguzi. Nashangaa kwa nini polisi hawakuwachukulia hatua walipokuwa wakitoa matamshi na vitendo vya vitisho,” amesema Museveni.

Lakini kauli hizo zimekosolewa vikali na wanaharakati wa demokrasia, wakisema zinachochea mazingira ya hofu, ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za kisiasa. Mwanaharakati Miria Matembe amemlaumu Rais Museveni kwa kile alichokitaja kuwa ni kuendelea kuwandama wapinzani wake hata baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi.

"Kwa nini wapinzani wanaoonyesha uwezo wa kuchukua mamlaka lazima wateswe, wauawe au watekwe? Je, hii ndiyo Uganda uliyopigania ukiwa kijana ulipoenda porini kutukomboa dhidi ya matatizo yaliyokuwa yanatuhangaisha,” Matembe ameuliza.

Bobi Wine mafichoni

Kwa sasa, Bobi Wine anaripotiwa kuwa bado yuko mafichoni, huku viongozi wawili wa chama chake, ambao ni manaibu wake wa kikanda, Dkt. Lina Zedriga na Jackline Jolly Tukamushaba, wakiripotiwa kutekwa nyara na kutofahamika waliko. Makamu mwingine, Muwanga Kivumbi, alikamatwa wiki iliyopita na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi na uhaini.

Bobi Wine: Hatutavumilia hujuma zozote kwenye uchaguzi

Aidha, mwishoni mwa wiki, vikosi vya usalama vilivamia makazi ya Bobi Wine. Kwa mujibu wa mkewe, ambaye bado amelazwa hospitalini, askari walimhujumu, wakaharibu nyumba kwa kuvunja milango na samani, na kuchukua mali mbalimbali ikiwemo simu za mkononi. Serikali hata hivyo imekanusha madai kuwa Bobi Wine analengwa kukamatwa.

Soma pia Uchaguzi wa Uganda kama jaribio la nguvu na mamlaka.

"Bobi Wine kusema kuwa yuko mafichoni hana sababu. Hakuna anayemwandama. Hawindwi na polisi, majeshi wala utawala. Kama msemaji wa serikali ya Uganda, nasema yuko huru kutoka alikojificha na arudi nyumbani kwake,” alisema Chris Baryomunsi.

Mitandao ya kijamii yafunguliwa Uganda

Katika hatua nyingine, mitandao ya kijamii imefunguliwa kikamilifu baada ya kufungwa kwa siku 13. Ingawa intaneti ilifunguliwa wiki iliyopita, wananchi wengi waliendelea kutumia mitandao ya VPN kuwasiliana.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, mkurugenzi wa mamlaka ya mawasiliano Nyombi Thembo alisema serikali imejiridhisha kuwa mitandao ya kijamii sasa inatumiwa kwa uwajibikaji na hakuna tena vitisho vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.