Mshambuliaji aua 50 na kujeruhi zaidi ya 400 Las Vegas | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mshambuliaji aua 50 na kujeruhi zaidi ya 400 Las Vegas

Watu 50 wameuawa na wengine zaidi ya 400 kujeruhiwa katika tukio la mashambulizi la risasi la watu wengi mjini Las Vegas Marekani. Shambulio hilo limeelezwa kuwa baya zaidi la watu wengi katika historia ya Marekani.

Mwanaume mmoja  aliejihami kwa silaha nzito ameuawa watu wasiopungua 50 na kuwajeruhi zaidi ya 400 katika tamasha la muziki mjini Las Vegas Marekani siku ya Jumapili, kwa kuwamiminia risasi kutokea ghorofa ya 32 ya jengo la hoteli lililo mkabala na saehemu lilikofanyika tamasha hilo.

Idadi hiyo ya vifo ambayo polisi imesisitiza ni ya awali, inalifanya shambulio hilo kuwa tukio kubwa zaidi ya mauaji ya risasi ya watu wengi katika historia ya Marekani, likipita lile la mwaka jana la mauaji ya watu 49 katika klabu cha usiku mjini Orlando.

Karibu watu 22,000 walikuwa katika mkusanyiko wakati mwanaume huyo alipoanza kufyatua risasi na kupelekea watu waliotaharuki kuanza kukimbia hovyo, na wakati mwingine kukanyagana wakati maafisa usalama wakihangaika kutafuta mahala zilikotokea risasi hizo.

USA - Schießerei in Las Vegas - Polizeieinsatz (Getty Images/E. Miller)

Askari polisi wakisaidiana na maafisa wa afya wanaomhudumia mmoja wa waathirika wa shambulio hilo.

Polisi mjini Las Vegas imesema watu wasiopungua 406 wamepelekwa katika hospitali za eneo hilo, na imemtaja mtuhumiwa kuwa mkaazi wa eneo hilo kwa jina Stephen Paddock mwenye umri wa miaka 64, lakini wameongeza kuwa hawana taarifa zaidi kuhusu lengo lake.

Mshambuliaji ajiuwa kabla ya kufikiwa na polisi

Paddock alijipiga risasi kabla ya polisi kuingia katika chumba chake cha hoteli alikokuwa akifyatulia risasi. Awali iliripotiwa kuwa Paddock, ambaye alikuwa na bunduki zaidi ya 10 chumbani kwake, aliuawa na polisi.

"Ni wazi kwamba hili tukio baya ambalo hatujawahi kushuhudia katika bonde hili. Kwa hivyo tutakachofanya ni vile tuwezavyo kuwaweka sawa maafisa wetu a kuazisha uchunguzi na kuhakikisha usalama wa jamii hii. Na tutafanya kila tuwezalo kurahishisha mnapata taarifa kama tunavyozijua," alisema kamanda wa polisi mjini Las Vegas Joseph Lombardo.

Awali maafisa walimtaja mwanamke aliekuwa chumba kimoja na Paddock kama mshukiwa, lakini baadae walisema hawamchukulii tena kuwa mhusika katika tukio hilo, viliripoti vituo vya televisheni vya CNN na Fox News. Picha za video zilizochukuliwa wakati wa shambulio hilo zimewaonyesha watu wakikimbia huku na kule kuokoa maisha wakati risasi zikiendelea kurindima mfululizo.

Steve Smith, mgeni aliekuja kuhudhuria tamasha hilo akitokea Phoenix, Arizona, aliielezea mirindimo ya risasi kama fataki, na kusema yumkini zilikuwa zinafyatuliwa risasi 100 kwa wakati mmoja. Kaka ya mshukiwa huyo Eric Paddock, amesema familia yao imeshtushwa na taarifa za alichokifanya ndugu yao.

President Trump über Las Vegas neu (Getty Images/A.Wong)

Rais Donald Trump akilihutubia taifa kufuatia mauaji ya Las Vegas, 02.10.2017.

Trump asema ni kitendo cha kishetani

Rais wa Marekani Donald Trump amezugumzia shambulizi hilo alilolitaja kuwa la kishetani, na kusema taifa limeungana leo katika huzuni na mshtuko. Akizungumza katika chumba cha diplomasia cha ikulu ya White House, Trump amesema atazuru Las Vegas siku ya Jumatano, kukutana na maafisa walioshughulikia shambulizi hilo pamoja na famila za waathirika.

Shambulio hilo limefanana na lile la mjini Paris Novemba 2015 ambamo watu 89 waliuawa, kama sehemu ya mashambulizi ya kupanga ya kundi la Dola la Kiislamu ambayo kwa jumla yalisababisha vifo vya watu 130.  Kundi hilo limedai kuhusika pia na shambulizi la sasa, lakini maafisa wa Marekani wamesema hakuna ushahidi kuhusu madai hayo ya IS.

Tamasha hilo lilifanyika katika eneo la wazi linalofahamika kama Las vegas village, mkabala na hoteli za Mandalay Bay na Luxor.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, afpe,dpae,afpe.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com