Mlinzi wa miaka 100 wa enzi ya Manazi kushitakiwa kwa mauaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mlinzi wa miaka 100 wa enzi ya Manazi kushitakiwa kwa mauaji

Mlinzi wa zamani wa kambi ya mateso aliye na miaka 100 anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kuchangia mauaji ya zaidi ya watu 3000 katika kambi ya mateso ya Sachsenhausen.

Waendesha mashitaka wamesema mwanamume huyo mzee mwenye umri wa miaka 100, mwanachama wa walinzi wa utawala wa kinazi SS anashitakiwa kwa makosa ya kusaidia kufanikisha mauaji ya watu 3,518 katika kambi ya Sachsenhausen iliyoendeshwa na utawala wa kinazi, wakati wa vita vya pili vya dunia, wakati alipokua mlinzi katika kambi hiyo kati ya mwaka 1942 na mwaka 1945.

Madaktari wamesema mshtakiwa ambaye hakutajwa jina, kutokana na sheria za ujerumani za kuripoti kesi za uhalifu mahakamani, hayupo katika hali nzuri sana kiafya kwa hiyo vikao katika kesi hiyo vitafanyika kwa masaa mawili na nusu kwa siku.

Kulingana na waendesha mashitaka, makosa mengine anayokabiliwa nayo ni kuwapiga risasi wafungwa wa vita katika eneo la kisovieti na kuwauwa wengine kwa kutumia gesi ya sumu ya Zyklon B iliyotumika pia katika kambi ya Auschwitz ambako mamilioni ya wayahudi waliuwawa.

Zaidi ya watu 200,000 walizuiliwa katika kambi ya mateso ya Sachsenhausen kati ya mwaka 1936 na 1945. Maelfu walikufa pia kwa kunyimwa chakula, magonjwa na kazi za kulazimishwa.

Mwanamume huyo mzee pia anakabiliwa na makosa ya mauaji ya kikatili

Ausstellung Kunstsammlung der Gedenkstätte Sachsenhausen

Picha ya kumbukumbu inyoonyesha baadhi ya mateso katika kambi ya Sachsenhausen

Taarifa ya mahakama ya Neuruppin iliyo karibu na mji wa Berlin, inayosikiliza kesi hiyo imesema babu huyo anashitakiwa kwa makosa ya kuchangia mauaji ya kikatili na kuchangia pia kuweka mazingira ya kuhatarisha maisha katika kambi ya Sachsenhausen.

Katika miaka kadhaa iliyopita kumeshuhudiwa kesi za uhalifu zikifunguliwa dhidi ya wazee waliokuwa walinzi katika kambi hiyo wanaoshitakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu uliofanyika wakati wa vita vya pili vya dunia. Wiki iliyopita bibi wa miaka 96 aliyekuwa karani katika kambi hiyo alitoroka siku ya kusikilizwa kwa kesi yake lakini baadae alikamatwa na polisi.

Uamuzi wa mahakama uliyopitishwa mwaka 2011, uliweka wazi kwamba, hata wale waliochangia mauaji wakati wa vita, sio lazima yawe moja kwa moja kwa moja ni lazima wawajibishwe.

Sachsenhausen, ilifunguliwa mwaka 1963 kama moja ya kambi za mwanzo kabisa za mateso za utawala wa kinazi. Ilikuwa kambi ya mafunzo kwa walinzi wa SS ambao baadae walikwenda kuhudumu katika kambi nyengine ya Auschwitz na Treblinka.

Chanzo: afp/reuters