1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa genge Haiti atishia kuwaua mateka wamishonari

22 Oktoba 2021

Kiongozi wa genge la wahalifu nchini Haiti lililowateka nyara kundi la wamishonari wa Kimarekani mwishoni mwa juma lililopita, ametishia kuwaua kulingana na video iliyoonekana na shirika la habari la AFP.

https://p.dw.com/p/4211y
USA | Christian Aid Ministries
Picha: AARON JOSEFCZYK/REUTERS

Video hiyo iliyochukuliwa Jumatano na kuchapishwa jana Alhamisi kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha Wilson Joseph, akiwa amevaa suti na kuzungukwa na watu wenye silaha, wakiwa mbele ya majeneza yaliyokuwa na miili ya wanachama watano wa genge lake.

Kiongozi huyo wa genge la wahalifu ametishia kuwaua Wamishonari hao kwa kuwa bado hajapata alichokihitaji. Vyanzo vya usalama vimeliambia shirika la habari la AFP kuwa watekaji nyara hao wanadai fedha cha dola milioni 17 ili kuwaachilia huru mateka.

Siku ya Jumamosi, kundi la wamishonari 17 wakiwemo raia wa Marekani na Canada pamoja na watoto wao walitekwa nyara walipokuwa wamekitembelea kituo cha watoto yatima mashariki mwa Port-au-Prince.

Marekani imetoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kusafiri Haiti kutokana na matukio ya utekaji nyara yanayolenga raia wa Marekani.