Mkutano wa Davos waanza Uswisi | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa Davos waanza Uswisi

Rais wa China Xi Jinping kufungua mkutano huo ambapo hotuba yake italenga kutetea utandawazi na biashara huru kati ya mataifa

 

Mkutano wa kimataifa wa kiuchumi unaofanyika kila mwaka katika mji wa mapumziko wa Davos nchini Uswisi, unaanza leo. Mkutano huo unaowaleta pamoja zaidi ya wakuu 100 wa mashirika makuu duniani unafunguliwa rasmi na Rais wa China Xi Jinping.

Hotuba ya Rais Xi Jinping katika ufunguzi wa kikao cha leo inatizamwa kuwa kilele cha mkutano huo na kwa nchi za Ulaya na Uswisi. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa rais wa nchi ya pili kwa ukubwa kiuchumi baada ya Marekani kuhudhuria mkutano huo wa kila mwaka unaowaleta pamoja viongozi wa nchi na wakurugenzi wakuu wa mashirika.

Hotuba ya Xi itakayolenga kuimarisha amani ulimwenguni, kukuza maendeleo kwa pamoja na mfumo wa biashara iliyo wazi kwa wote ulimwenguni, inajiri wakati kukiwa na hofu kuwa rais ajaye wa Marekani Donald Trump huenda akaweka mikakati ya kukuza biashara za kibinafsi badala ya biashara huru na mataifa mengine.

Klaus Schwab

Klaus Schwab

Akizungumza na wanahabari nchini Uswisi kabla ya mkutano, Xi alisema atatetea utawala ulio sawa na mwelekeo mwema duniani. Klaus Schwab ambaye ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Jukwaa hilo la kiuchumi amesema ana matumaini mkutano utapata suluhisho kwa baadhi ya matatizo."Tunakutana wakati kuna mkanganyiko tele na maswali mengi sana. Tunayopaswa kuyafanya hapa ni kushughulikia vyanzo vya wasiwasi. Ninatarajia mjadala wenye ari unaolenga kupata suluhisho kwa pamoja."

Mwakilishi pekee wa Donald Trump Anthony Scaramucci ambaye ni mshauri wake mkuu anatarajiwa kuelezea mkutano huo vipaumbele vya utawala wa Trump. Mkutano wa Davos unajiri wakati wanademokrasia katika nchi za magharibi wanakabiliana na kuibuka kwa ushawishi wa kizalendo, ikiwemo uliomsaidia Donald Trump kutwaa mamlaka. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni Uongozi wa uwajibikaji.

Eneo linakofanywa mkutano wa Davos

Eneo linakofanywa mkutano wa Davos

China ilitizamiwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono Jukwaa la Kimataifa la Kiuchumi WEF, baada ya Trump kusema ataondoa Marekani katika jumuiya ya kibiashara ya nchi kumi na mbili wanachama wa biashara ya Pasifik iliyoanzishwa na Rais Barrack Obama.

Urusi pia itawakilishwa na manaibu wawili wa waziri mkuu na wakuu wengine wa kibiashara. Washiriki 3,000 miongoni mwao wanasiasa, wakuu wa biashara, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, wasomi na wanaharakati, wanatarajiwa kujadili masuala ya kiulimwengu yanayoweza kukabiliana na siasa za umaarufu, ukosefu wa usawa katika maendeleo ya teknolojia na kupungua kwa nafasi za ajira.

Mwandishi: John Juma/DPAE/RTRE/APE

Mhariri: Josephat Charo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com