Mjadala wa kumiliki bunduki wazua mgomo Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mjadala wa kumiliki bunduki wazua mgomo Marekani

Mgomo ndani ya baraza la wawakilishi nchini Marekani umeendelea baada ya wabunge wa chama cha Republican kukataa takwa la wawakilishi wa Democratic kwamba mswada wa kudhibiti umiliki wa bunduki Marekani upigiwe kura.

Wawakilishi wa Democratic wakigoma katika baraza la wawakilishi.

Wawakilishi wa Democratic wakigoma katika baraza la wawakilishi.

Mgomo ndani ya baraza la wawakilishi nchini Marekani umeendelea leo baada ya wabunge wa chama cha Republican kukataa matakwa ya wabunge wa chama cha Democratic. Hii ni hata baada ya wawakilishi wa Democratic kufanya mgomo ndani ya baraza hilo kushinikiza mjaadala kuhusu udhibiti wa umiliki wa bunduki nchini humo.

Kwa zaidi ya saa kumi na nne, wawakilishi kadhaa wa chama cha Democratic walimiminika katika baraza hilo na kukaa kwenye sakafu kama hatua ya kuwashinikiza wawakilishi wa chama cha Republican wakubali kuupigia kura muswaada wa kudhibiti umiliki wa bunduki nchini humo.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya shambulizi la Orlando ambapo takriban watu 50 waliuawa kwa kupigwa risasi. Hata hivyo wanarepublican wamepuuzilia mgomo huo na kusema kuwa ni mpango wa kujipatia umaarufu mbele ya Wamarekani.

Spika Paul Ryan alikataa matakwa ya wanademocrat kuhusu umiliki wa bunduki na badala yake kulazimisha kuura kuhusu mswada tofauti. Spika Ryan anasema "Spika anatambua kuwa wawakilishi watatofautiana kuhusu masuala ya sera na watataka kuelezea tofauti zao. Lakini spika atatumai kuwa shughuli za baraza zifanywe kwa nidhamu inayokuza heshima na hadhi ya baraza tunalotumikia sote."

Wawakilishi wa Democratic wakigoma katika baraza la wawakilishi.

Wawakilishi wa Democratic wakigoma katika baraza la wawakilishi.

Vikao vya baraza vyaahirishwa

Mgomo huo ulilazimisha baraza kukatisha shughuli zake hadi pale spika atakapoitisha vikao vingine tena. Wanademocrat wanashikilia kuwa wataendeleza mgomo huo hadi matakwa yao yaitikiwe. Mgomo huu unaenda sambamba na hatua ya wabunge wa democrat katika seneti wiki jana kulalamikia kutochukuliwa kwa hatua madhubuti kuhusu udhibiti wa umiliki wa bunduki.

Mjadala kuhusu umiliki wa bunduki umekuwa suala kuu la kisiasa nchini Marekani, hasa ikizingatiwa kumekuwa na misururu ya mauaji yanayofanywa na wanaomiliki bunduki nchini humo. Steny Hoyer ni kiongozi wa waliowachache katika baraza la wawakilishi na anasema. "Huu mjadala ni kuhusu kuhakikisha wale wasiofaa kumilika bunduki hawamiliki bunduki. Ndiyo sababu tuko katika sakafu hii, kusema ikiwa tumebaini kuwa wewe ni hatari kusafiri kwa ndege, basi wewe ni hatari zaidi kuwa na bunduki"

Nje ya baraza hilo, raia wanaounga mkono wito wa kuwepo kwa sheria za kudhibiti umiliki wa bunduki miongoni mwa raia nchini Marekani, walipiga kambi wakiwa na mabango ya wito huo.

Mwandishi: John Juma/RTRE/

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com