Miaka 30 tangu CDU/CSU waanze kushirikiana na FDP | Magazetini | DW | 25.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Miaka 30 tangu CDU/CSU waanze kushirikiana na FDP

Miaka 30 tangu CDU/CSU walipounda serikali kuu pamoja na chama kidogo cha kiliberali FDP na pendekezo la chama cha upinzani cha SPD kuhusu malipo ya uzeeni ni mada zilizohanikiza magazetini nchini Ujerumani.

Kansela wa zamani Helmut Kohl na mpya Angela Merkel

Kansela wa zamani Helmut Kohl na mpya Angela Merkel

Tuanze lakini na jinsi wahariri wanavyoangalia maandalizi ya sherehe za kuadhimisha miaka 30 tangu CDU/CSU walipoanza kushirikiana kwa mara ya kwanza madarakani na waliberali wa FDP.Gazeti la Saarbrücker Zeitung linaandika:

Wananchi hawahitaji shamra shamra hizo.Kwasababu bado wanayo picha waliyojichorea wenyewe kumhusu kansela aliyeongoza serikali ya kwanza ya muungano wa CDU/CSU na FDP-Helmut Kohl.Na picha hiyo inatatanisha.CDU ndio wanaomhitaji Helmut Kohl kama mhimili wao uliotukuka.Pengine wangemwangalia kama kiumbe tu ingekuwa bora zaidi.Angela Merkel pia ni kiongozi aliyekomaa ingawa si desturi yake kujishughulishi na makundi yanayopalilia mivutano chamani,kama alivyokuwa akifanya Helmut Kohl.Bora hivyo.

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linahisi sherehe za miaka 30 tangu ilipoundwa kwa mara ya kwanza serikali ya muungano ya CDU/CSU na waliberali wa FDP zina walakin.Gazeti linaendelea kuandika:

Sherehe CDU wanazotaka kumfanyia Helmut Kohl wiki hii,zina walakin.Kwasababu anatumiwa mtu ambae ni hohe hahe.Na hata kusema hawezi.Picha za kusisimua bila ya shaka zitatolewa..Wananchi hawahitaji lakini sherehe kama hizo.Kwasababu sio tu miaka hiyo 30 ya serikali ya muungano bado haijaingia katika daftari la kumbukumbu za taifa,lakini pia kwasababu wengi wa wananchi wana picha yao wenyewe ya jinsi wanmavyomuangalia kansela huyo na picha hiyo inatatanisha.

Portrait Alt-Bundeskanzler Helmut Kohl

Helmut Kohl

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na pendekezo la chama cha upinzani cha SPD kuhusu malipo ya uzeeni.Suala wahariri wanalojiuliza ni jee pendekezo hilo litakubaliwa na wote miongoni mwa wafuasi wa chama hicho?Gazeti la "Landeszeitung linaandika:

Sigmar Gabriel anaweza kujifaharisha kama muasisi wa mfumo mpya wa malipo ya uzeeni wa chama cha Social Democratic.Lakini kimya chake,licha ya pendekezo lake kupata uungaji mkono bayana wa chama chake,si cha bure:Anahofia zisije zikawa mbio za sakafuni.Anahofia wakati wa mkutano mkuu,mwezi November mwaka huu,wafuasi wa mrengo wa shoto wa chama hicho wasije wakalipinga:Kwasababu hapo madhara hayatamkumba yeye Gabriel kama mwenyekiti wa chama cha SPD tu, suala zima la nani anastahiki kugombea kiti cha kansela kwa tikiti ya SPD litakuwa limepitwa na wakati.

Nalo gazeti la "Braunschweiger Zeitung" linaandika:

Jibu la kitisho cha umaskini wa uzeeni haliwezi kupatikana katika malipo ya uzeeni ya serikali peke yake.Na hapo Sigmar Gabriel hajakosea hata kidogo.Lakini anaweza kuwatanabahisha wenzake wote chamani?Kwasababu SPD inalemazwa na mambo mawili:kwanza mvutano usiokwisha chamani na pili kuhusu mgombea wa kiti cha kansela.Frank-Walter Steinmeier au Peer Steinbrück hawatojitangaza rasmi ikiwa hawana hakika kama chama chao kiko tayari kujifanyia marekebisho.Kwa hivyo sio pekee suala la malipo ya uzeeni na wala si suala la nani awe mgombea wa kiti cha kansela-hakauna kinachofuata njia kwa sasa katika chama cha SPD.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman