Mgogoro Kati ya Urusi na Uturuki wazidi kufukuta | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mgogoro Kati ya Urusi na Uturuki wazidi kufukuta

Rais Putin ameagiza kuwekwa mifumo ya kuzuia makombora katika kambi ya kijeshi ya Urusi nchini Syria,hatua ambayo imeongeza kitisho cha kutokea makabiliano ya kijeshi kati ya nchi hiyo na Uturuki:.

Ndege ya kivita ya Urussi iliyoangushwa na Uturuki

Ndege ya kivita ya Urussi iliyoangushwa na Uturuki

Wakati hali ya kurushiana lawama ikiendelea kushuhudiwa katika mvutano uliojitokeza kati ya Urusi na Uturuki kufuatia kuangushwa kwa ndege ya kivita ya Urusi,rais Vladmir Putin ameagiza kuwekwa mifumo ya kuzuia makombora katika kambi ya kijeshi ya Urusi nchini Syria,hatua ambayo imeongeza kitisho cha kutokea makabiliano ya kijeshi kati ya nchi hiyo ya Uturuki ambayo ni mwanachama wa NATO na Urusi.

Mifumo ya kuzuia makombora aina ya S-400 ya Urusi itapelekwa katika kambi ya kijeshi ya Hemeimeem katika mkoa wa pwani ya Latakia nchini Syria ikiwa ni kilomita 50 kutoka mpaka kusini mwa mpaka wa Uturuki. Mifumo hiyo ya kuzuia makombora ina uwezo wa kuzilenga ndege za kivita za Uturuki na kuziangamiza kabisa.Ikiwa hilo litatokea basi inamaana Jumuiya ya Kujihami ya NATO itahitajika kuingilia kati.

Rais Vladimir Putin

Rais Vladimir Putin

Uturuki iliiangusha ndege ya kivita ya Urusi aina ya Su-24 siku ya Jumanne ikisema ndege hiyo iliingia kwenye anga yake ikitokea Syria licha ya kupewa onyo mara kadhaa.Rubani mmoja wa ndege hiyo aliuwawa na wanamgambo baada ya kuchupa nje na mwavuli huku mwenzake akiokolewa na makomando wa jeshi la Syria na kukabidhiwa akiwa katika hali nzuri ya afya kwa wanajeshi wenzake katika kambi ya kijeshi ya Urusi siku ya Jumatano.

Rais Putin alighadhabishwa na tukio hilo alilosema ni sawa na kitendo cha kuichoma kisu mgongoni na kuwa ni uhalifu na unafiki akioonya nchi hiyo juu ya athari zitakazosababishwa na tukio hilo.Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema mifumo ya ulinzi wa makombora ya Urusi iko njiani kuelekea pwani ya Latakia ambako ni karibu na mpaka wa Uturuki yakinuiwa kuzilinda ndege za kivita za Urusi.

Ameweka wazi kwamba mifumo hiyo ya kuzuia makombora itakuwa tayari kuharibu chombo chochote kitakachoonekana kusababisha hatari kwa ndege za Urusi.Pamoja na hayo amesema kuanzia sasa wanajeshi wote wa Urusi wa kufyetua mabomu watasindikizwa na ndege za kivita katika operesheni zao za Syria.

Viongozi wa Uturuki rais Tayyip Ergodan na waziri mkuu Ahmet Davutoglu

Viongozi wa Uturuki rais Tayyip Ergodan na waziri mkuu Ahmet Davutoglu

Kwa upande mwingine wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imetoa taarifa ikisema waziri wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wamekubaliana kukutana siku chache zijazo baada ya kuzungumzwa kwa njia ya simu hii leo ingawa Lavrov amesema hana mpango kama huo.

Na kama hilo halitoshi waziri mkuu wa Uturuki ameikosoa Urusi na operesheni zake Syria na hasa katika jimbo la Turkimenistan akisema katika eneo hilo hakuna mpiganaji hata mmoja wa kundi la IS na kwahivyo ameitaka Urusi isimamishe operesheni zake kwenye eneo hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com