1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfahamu Annegret Kramp-Karrenbauer, kiongozi mpya wa CDU

Daniel Gakuba
7 Desemba 2018

Chama cha Christian Democratic Union kinachoongoza serikali ya mseto ya Ujerumani kimemchagua Annegret Kramp-Karrenbauer kuwa mwenyekiti wake mpya. DW inatazama safari yake hadi kufika katika wadhifa huo muhimu.

https://p.dw.com/p/39giM
Annegret Kramp-Karrenbauer speaks at the press conference in Berlin - 07 Nov 2018
Picha: picture alliance

Safari ya mwenyekiti mpya wa chama cha CDU, Annegret Kramp-Karrenbauer ni mithili la somo kuhusu umuhimu wa kuwa mahali muafaka kwa wakati ufaao kisiasa.

Miaka 2 iliyopita, AKK kama ajulikanavyo kwa kifupi alikuwa waziri kiongozi wa jimbo dogo la Saarland lililo Kusini Magharibi mwa Ujerumani, akikabiliwa na kibarua kigumu cha kuchaguliwa tena. Miezi 24 baadaye, anachukua nafasi ya shujaa wake kisiasa, Angela Merkel kama mwenyekiti wa chama kikubwa zaidi Ujerumani, chenye historia ya kudhibitiwa na wanaume.

Katika mkutano mkuu wa chama cha CDU mjini Hamburg Ijumaa, Kramp-Karrenbauer alijinadi kama mgombea kwa ajili ya umoja na mwendelezo wa sera za chama hicho wakati huu.''Hakuna wahafidhina wala waliberali, kuna CDU peke yake,'' alisema.

Angela Merkel und Annegret Kramp-Karrenbauer
Kramp-Karrenbauer ni mshirika wa karibu wa Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Nyota yake ilianza kung'ara Machi 2017, alipokiongoza chama chake kupata ushindi wa asilimia 40.7 jimboni Saarland, wakati ambapo mgombea wa chama cha Social Democratic, SPD Martin Schulz alikuwa akivuma katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura. Ni AKK ambaye alianzisha upepo ulioipindua meli ya Schulz, na kupanda mara moja kwenye jukwaa la kitaifa.

Mwanzo mgumu jimboni Saarland

Kramp-Karrenbauer mwenye umri wa miaka 56 alizaliwa katika kijiji kidogo cha Voelklingen na alikulia katika mji mdogo wa Puettlingen. Baba yake alikuwa mwalimu, na mama yake alikuwa mama wa nyumbani. Kama ilivyo kwa watu wengi wa jimbo hilo, yeye ni Mkatoliki, na anao watoto watatu.

Alijiunga na CDU mwaka 1981 katika tawi la vijana, na akapanda taratibu hadi wadhifa wa mwenyekiti wa chama hicho katika jimbo la Saarland mwaka 2011, akiwa mwanamke wa kwanza kuuchukua. Wakati huo alishinda kwa kishindo kwa asilimia 97.

Kuanzia 2001 hadi 2004 alikuwa pia mwanamke wa kwanza kuteuliwa waziri wa mambo ya ndani wa jimbo lake. Mwaka 2011 alifanikiwa kuunda muungano na vyama vingine; cha Kijani na cha Free Democrats, FDP na kuchaguliwa kuwa waziri kiongozi wa Saarland.

Baada ya kuchaguliwa tena mwaka 2007, alikanusha tetesi kwamba alikuwa na ndoto za kuingia kwenye uwanja wa shirikisho, akisema anaridhika na kuliongoza jimbo lake. Lakini, mwaka mmoja baadaye, aliitikia wito wa Kansela Angela Merkel wa kuwa Katibu Mkuu wa CDU kitaifa, akaidhinishwa Februari mwaka huu wa 2018.

Mhafidhina wa mrengo wa kati

Miongoni mwa wagombea watatu waliowania uenyekiti wa CDU katika mkutano mkuu wa Hamburg, AKK alitazamwa kama mwenye msimamo unaorandana na wa Merkel. Akina mama hao wamefanya kazi pamoja, na Kramp-Karrenbauer akadhihirisha kuwa mtu asiyependa makuu, kama Angela Merkel. Lakini lihusikapo suala la wahamiaji, yeye anao msimamo mkali zaidi kuliko Merkel.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mkutano wa Ijumaa, AKK alikiri kwamba suala la wahamiaji ni muhimu, lakini akaongeza, ''Ikiwa unadhani tutakuwa na mjadala wa kubadilisha kilichotokea mwaka 2015 (mmiminiko wa wakimbizi), tuambiazane ukweli, matukio hayo ni hali halisi, hayabadiliki.''

Alisema kilicho muhimu ni kuhakikisha tukio la mwaka 2015 halitokei tena, akiongeza kuwa alichangia katika kuhakikisha hilo alipokuwa kiongozi kwenye ngazi ya jimbo.

Ikiwa kauli yake hiyo itawaridhisha wanachama waliopendelea mtazamo wa kihafidhina zaidi katika chama chake kuhusu suala la wahamiaji, ni jambo la kusubiri na kuona. Hilo hata yeye Kramp-Karrenbauer analitambua, na licha ya kuwa karibu sana na Kansela Merkel, anahitaji kujijenga kama mwenyekiti anayeweza kuunganisha chama kilichogawika, baada ya uongozi wa Merkel.

Mwandishi: Jefferson Chase

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Nancy Isenson