1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Israel na Misri wakutana

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
30 Mei 2021

Maafisa wa ngazi za juu wa Misri na Israel wamekutana kwa mazungumzo kuhusu kuyatilia mkazo makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Israel na kundi la kundi la Hamas.

https://p.dw.com/p/3uBk3
Kairo Israelische Außenminister Gabi Aschkenasi in Ägypten zu Besuch
Picha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Mazungumzo hayo pia yamehusu namna ya kuujenga upya Ukanda wa Gaza baada ya mashambulio ya siku 11 yaliyosababisha uharibifu mkubwa kwenye eneo hilo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gabi Ashkenazi aliwasili mjini Cairo, Misri siku ya Jumapili kwa ajili ya kufganya mazungumzo na mwenzake Sameh Shoukri.

Soma zaidi:Baada ya vita Gaza, wakaazi wakabiliwa na masaibu yale yake

Safari hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel nchini Misri ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa wadhfa huo kutoka Israel kwa muda wa miaka 13 iliyopita. Ashkenazi amesema katika mazungumzo yao na mwenzake wa Misri pamoja na kuujenga upya Ukanda watazungumzia pia juu ya uwezekano wa kupatikana makubaliano ya kudumu ya kusimamisha mapigano na kundi la Hamas linaloudhibiti Ukanda wa Gaza. Vilevile watajadili juu ya mikakatiu ya kuwafikishia misaada watu wa Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Ahmed Gharabli/AFP

Mamlaka ya Palestina imekisia mamilioni ya dola yatakayohitajika katika ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza na kwa upande wake Israel imeanza kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na makombora yaliyorushwa na wapiganaji wa kundi la Hamas. Wapalestina wapatao 248 waliuawa kwenye mzozo huo ambapo raia wa Israel 13 nao waliuawa.

Misri ambayo inapakana na Ukanda wa Gaza imekuwa mstari wa mbele katika maswala ya usuluhishi baina ya pande mbili za Israel na Hamas kwa muda mrefu. Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na mkuu wa usalama wa Misri Abbas Kamel mjini Jerusalem na wamejadili juu ya mwaswala ya usalama yanayohusu kanda ya Mashariki ya Kati.

Baadhi ya maeneo ya Gaza yaliyoharibiwa kwenye mapigano
Baadhi ya maeneo ya Gaza yaliyoharibiwa kwenye mapiganoPicha: Tania Kraemer/DW

Wote Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wake wa mambo ya Nje Gabi Ashkenazi wamesisitiza kuwa jambo la muhimu kwao na nchi yao ya Israel ni kufanikisha kuachiwa na kuweza kurudi nyumbani raia wawili wa Israel na pia miili ya askari wawili wa Israel ambayo inashikiliwa kwa mika mingi katika Ukanda wa Gaza. Kundi la Hamas mpaka sasa limegoma kuwaachia raia hao pamoja na miili hiyo ya askari wa Israel.

Soma zaidi:UN: Mashambulizi ya Gaza huenda yakachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita

Misri ilifaulu kuzipatanisha Israel na Hamas kusimamisha mapigano katika makubaliano ambayo bado yanaendelea hadi sasa tangu yalipofikiwa hapo tarehe 21, Mei. Ni mafanikio ya kidiplomasia ambayo yanafuatiliwa na wengi, Misri inashirikiana na Marekani na washirika wengine wa kikanda katika juhudi za kufanikisha usitishaja kudumu wa vita kati ya Israel na kundi la Hamas.

Vyanzo:DPA/RTRE/AP