Matumaini yachomoza Brussels | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Matumaini yachomoza Brussels

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubiliana kukabiliana na migogoro ya fedha na kuimarisha msingi wa umoja wa uchumi na sarafu kwa kuanzisha mkakati wa kusimamia shughuli za benki za nchi wanachama wa Umoja huo.

Picha ya viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya

Picha ya viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya

Baada ya zaidi ya masaa manane ya majadiliano, viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya wameahidi kusonga mbele na juhudi zao za kubuni mkakati wa kukabiliana na matatizo yanayozikaba benki ingawa haikuwa dhahiri lini mkakati huo utakamilika.

"Tumekubaliana kuhusu muongozo wa siku za mbele wa umoja wa sarafu," amesema kansela wa Ujerumani, Angela Merkel mbele ya waandishi habari bila ya kutoa maelezo zaidi..

Wameanzisha pia mijadala juu ya jinsi nchi zinavyoweza kufuata malengo yaliyowekwa ya kiuchumi na kubuni "fuko la mshikamano ili kuyasaidia mataifa yanayosumbuliwa na migogoro ya fedha.

Merkel PK beim EU Gipfel in Brüssel

Kansela Angela Merkel akizungumza na waandishi habari mjini Brussels

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametoa mwito makubaliano yafikiwe hadi mwezi Juni mwakani. Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, anashauri awamu ya kwanza ya mkakati huo wa kusimamia shughuli za benki ianze mwishoni mwa mwaka 2013 na ya pili mapema mwaka 2014. Lengo ni kuona mkakati huo unapitishwa na bunge la sasa la Ulaya.

Spika wa bunge la Ulaya, Martin Schulz, ambaye alishiriki hapo awali mazungumzoni anasema:"Huu ni msingi wa majadiliano ya miezi kadhaa kuhusu wapi, lini na vipi madeni ya mataifa wanachama yanaweza kudhaminiwa kwa pamoja . Naamini huu ndio msingi ambao tumekuwa tukiushughulikia tangu muda mrefu sasa."

Kansela Merkel amefafanua mkakati mzima jinsi utakavyofanya kazi katika daraja ya Ulaya na akasisitiza kwamba "haupaswi kuangukia mabegani mwa walipa kodi."

Mkutano huo wa siku mbili wa viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya, wa sita na wa mwisho kwa mwaka huu wa 2012, ulilenga tangu mwanzo kusaka njia bora za kupambana na mgogoro wa kiuchumi na kurekebisha matatizo yaliyosababishwa na miaka mitatu ya mgogoro wa madeni.

Infografik Karte EU und dei EURO-Zone englisch ENG

Ramani ya nchi wanachama wa zoni ya Euro

Mkutano wa viongozi umefanyika saa chache baada ya mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya kufikia makubaliano kuhusu "umoja wa benki" kwa kukubaliana kwamba benki kuu ya Ulaya ndiyo itakayosimamia shughuli za benki ya kanda ya Euro.

Uamuzi huo pamoja na maamuzi mengine yaliyofikiwa na mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro kuipatia Ugiriki msaada mwengine wa Euro bilioni 50 ndio matokeo ya maana yaliyofikiwa hadi wakati huu. Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unaendelea hii leo mjini Brussels.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com