1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya mashabiki kurejea uwajani Ujerumani yayeyuka

Deo Kaji Makomba
10 Agosti 2020

Matumaini ya vilabu vya soka vya Ujerumani kwa mashabiki wake kurejea uwanjani yameyeyuka baada ya mkutano wa afya kutupilia mbali uwezekano huo.

https://p.dw.com/p/3gkon
DFB (Deutscher Fussball Bund) Logo, Wappen, Schriftzug vor Zentrale
Picha: picture-alliance/HMB Media/O. Mueller

Matumaini ya vilabu vya soka vinavyoshiriki ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga kuhusu kurejea kwa uchache viwanjani kwa mashabiki wao wakati msimu mpya wa ligi hiyo utakapoanza mnamo Septemba 18 mwaka huu, yameyeyuka.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, vilabu 36 katika ligi kubwa mbili za juu nchini Ujerumani zilikubaliana vipengele vinne vya mapendekezo kutoka katika bodi ya ligi, DFL, ambavyo vingewezesha kuona mashabiki wakirejea viwanjani licha ya kuwepo na mlipuko wa virusi vya Corona.

Vilabu vilikubaliana kuuza tiketi za kibinafsi kwa ajili ya kufuatilia watazamaji, na hakuna mashabiki kutoka timu pinzani kwa mwaka 2020, hakuna pombe iliyoruhusiwa hadi mwezi Oktoba na mashabiki wakiwa wameketi tu kwenye viti, na maeneo ya veranda uwanjani yakibaki wazi. Hata hivyo, lazima kwanza upitishwe na serikali ya Ujerumani.

Logo Fußball 1. Bundesliga DFL
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Mwanasiasa Dilek Kalayci, ambaye ni mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa afya wa Ujerumani waliokutana Jumatatu tarehe (10.08.2020) alimwaga maji baridi katika kwenye matumaini ya ligi hizo.

"Hatupo tayari kupitisha maamuzi juu ya dhana ya usafi wa DFL, "Kalayci aliliambia gazeti la Berliner Morgenpost kabla ya mkutano. "Kandanda la kulipwa halipo katika orodha ya vipaumbele vya kwanza kwa mawaziri wa afya.”


Vilabu vya soka vilivyoko katika ligi kuu ya soka nchini Ujerumani, vimepoteza mamilioni ya euro kwa kupoteza mapato yatokanayo na viingilio kwa kila mechi ya nyumbani zilizokuwa zikichezwa bila ya kuwa na mashabiki uwanjani.

Virtuelle Bundesliga
Picha: picture-alliance/dpa/G. Kirchner

Ingawa, idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona inaongezeka kidogo nchini Ujerumani na visa vipya 436 vikiripotiwa katika saa 24 zilizopita na jumla ya vifo karibu 9,000 vikiripotiwa.

Mechi tisa za mzunguko wa mwisho wa ligi ya Bundesliga katika msimu uliopita zote zilichezwa huku milango ya viwanja ikiwa imefungwa kuzuia mashabiki kuingia uwanjani. Frizt Keller, rais wa shirikisho la soka nchini Ujerumani, alipendekeza wazo la mashabiki kufanyiwa vipimo katika msimu ujao, lakini Kalayci akatupilia mbali wazo hilo.


"Wazo la kwamba, miongoni mwa vitu vingine, mashabiki wote viwanjani wanaweza kufanyiwa vipimo liliangaliwa kwa kupingwa na idadi kubwa ya mawaziri,”aliongeza Kalayci.

Chanzo: AFP