1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapiga marufuku makundi mawili ya DRC na Msumbiji

John Juma
11 Machi 2021

Marekani imeyaorodhesha makundi mawili ya wanamgambo wenye misimamo mikali kutoka Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo miongoni mwa makundi ya kigaidi kwa kuyahusisha na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, (IS). 

https://p.dw.com/p/3qTua
Kongo, Soldaten der FARDC
Picha: AFP/Getty Images/A. Wandimoyi

Kundi la wanamgambo kutoka Kongo Allied Democratic Forces (ADF) na kiongozi wake Seka Musa Baluku, na kundi la Msumbiji Ahlu Sunnah Wa-Jama pamoja na kiongozi wake Abu Yasir Hassan wamejumuishwa kwenye orodha hiyo na kutajwa haswa kama ”magaidi wa ulimwengu”.

Hatua hiyo inamaanisha wanachama wa makundi hayo hawaruhusiwi kusafiri kuelekea Marekani, mali zao zilizoko Marekani kushikiliwa na serikali, biashara na kampuni yoyote ya Marekani ni marufuku, na ni jinai kuyaunga mkono makundi hayo au kuyapa msaada wowote.

Marekani imeyapa makundi hayo majina ya IS-DRC na IS-Msumbiji.

Jeshi la DRC lilianza operesheni dhidi ya ADF mwaka 2019
Jeshi la DRC lilianza operesheni dhidi ya ADF mwaka 2019Picha: Reuters/Kenny Katombe

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kupitia taarifa yake kwamba mnamo Aprili mwaka 2019, kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS la nchini Iraq na Syria, lilitangaza kuanzisha tawi lake la Afrika ya Kati 'Islamic State Central Africa Province' (ISCAP), ili kuhakikisha uwepo wao na kuendeleza shughuli zao katika Afrika ya Kati, Mashariki na Kusini.

Wizara hiyo imeongeza kwamba japo vyombo vya habari vinavyofungamana na IS huangazia ISCAP kama kundi lililoungana, makundi ya IS-DRC na IS-Msumbiji ni makundi tofauti yenye asili tofauti. Makundi hayo yamefanya mashambulizi ya kigaidi au yanatishia kufanya matendo ya kigaidi.

Kundi la ADF ambalo ni la waasi kutoka Uganda, limekuwa likifanya mashambulizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu miaka ya 1990, na tangu jeshi lilipoanza operesheni dhidi yao mwaka 2019, kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi mabaya dhidi ya raia kulipiza kisasi.

Kundi la ADF limewaua mamia ya watu mashariki mwa DRC

Soma pia:

Kundi la ADF limekuwa likifanya mashambulizi na kuua mamia ya watu mashariki mwa DRC
Kundi la ADF limekuwa likifanya mashambulizi na kuua mamia ya watu mashariki mwa DRCPicha: Getty Images/AFP/K. Mailro

Mwaka huu pekee, wanamgambo wa ADF wameshutumiwa kwa kuwaua watu 140, kufuatia mashambulizi yao ya takriban kila wiki mashariki mwa Kongo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mwaka uliopita, kundi hilo liliwaua takriban watu 850.

Kundi la Ahlu Sunnah Wa-Jama ambalo linafahamika nchini Msumbiji kama Al-Shabaab lilifanya mashambulizi ya kwanza mwaka 2017, haswa kwa kuwachinja watu. Wapiganaji wake waliapa kushirikiana na IS mwaka 2019 na hadi leo, kundi hilo limezidisha mashambulizi yake.

Laren Poole ambaye ni afisa wa wakfu wa Marekani Bridgeway, amesema ufadhili kutoka kundi la IS kwa ADF, umeliimarisha kundi hilo kufanya mashambulizi hatari.

J3Congo army spokesman on ongoing operation against the ADF rebels in Beni. - MP3-Stereo

Wachambuzi watilia mashaka kama vikwazo vitakuwa na tija

Poole ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanaamini kwa kulenga fedha za kundi hilo pamoja na mitandao yake ya kusajili wanachama, ni njia imara kabisa ya kupunguza machafuko yanayofanywa IS katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi, wametilia mashaka uhusiano wowote kati ya ADF na IS.

Dan Fahey, ambaye ni mwanachama wa zamani wa kundi lililotwikwa jukumu la kufuatilia vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa DRC, amesema vikwazo hivyo vipya huenda visiwe na athari yoyote, sawa na vikwazo vilivyowekewa ADF mnamo mwaka 2014. Kulingana na Fahey, hatua hii ni ya ishara tu. Lakini inashangaza kwa sababu mara kwa mara kundi la wataalamu limepuuza hali na nguvu ya ushawishi wa IS nchini Kongo.

(RTRE)