1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa ADF watekeleza mauaji ya watu 46 Congo

Amina Mjahid
15 Januari 2021

Waasi kundi la ADF linaloendesha harakati zake mashariki mwa Congo, jana wameshambulia kijiji cha Masini katika wilaya ya Irumu,kasenyi mkoa wa Ituri Kaskazini mashariki ya Congo, na kuwauwa Mbilikimo 46.

https://p.dw.com/p/3nxIt
DR Kongo Alltagsleben in Beni in der nähe von dem Kreisverkehr Nyamwissi
Picha: DW/W. Bashi

Shambulizi hilo lilifanyika wakati Mbilikimo wanaume wakiwa wamekwenda katika mawindo msituni. Mbilikimo huyu alienusurika kimiujiza, anaelezea jinsi mambo yalivyokuwa.

"Walijitokeza na silaha na kufyetua risasi, huku wengine wakiwauwa watu hasa wanawake kwa kuwakata kwa mapanga. Na wanawake waliojaribu kutoroka, walipigwa risasi. Waliouawa ni wanawake pamoja na watoto."

Ripoti ya kuuawa kwa mbilikimo katika kijiji cha Masini, ilithibitishwa na mbunge wa kuchaguliwa wa wilaya ya Irumu Jackson Aussen,anaesema kwamba miili ya mbilikimo hao waliouawa haijazikwa bado.

"ADF walishambulia kambi ya mbilikimo na kuwauwa watu wote waliokuwemo kambini humo. Matokeo ni mabaya kabisa. Watu arubaini na sita waliuawa," alisema Jackson Aussen.

Wanaharakati wavunjwa moyo kutokana mashambulizi ya mara kwa mara

Demorkatische Republik Kongo - Soldaten der Democratic Republic of Congo nach Kämpfen mit Rebellen
Baadhi ya wanajeshi wa Congo wakiwategea waasi wa ADFPicha: Reuters/G. Tomsaevic

Mashambulizi ya ADF kila mara katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Irumu mkoani Ituri, na wilaya hiyo ikiwa jirani na ile ya Beni katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, yameshawavunja moyo wanaharakati wa haki za binaadamu.

Christophe Munyanderu, ni mratibu wa shirika la kutetea haki za Binaadamu CRDH katika wilaya ya Irumu, anaiomba serikali kutilia maanane usalama wa raia katika wilaya ya Irumu.

soma zaidi: Raia 20 wauwa kaskazini-mashariki mwa DRC

ADF wakiwa wanakabiliana na majeshi ya serikali katika wilaya ya Beni, mkoani Kivu ya Kaskazini,wameamuwa kuendesha Mashambulizi katika mkoa wa Ituri, ili kuwachanganya wanajeshi wanaopambana nao.

Aidha shambulizi la jana katika kijiji cha Masini katika wilaya ya Irumu, mkoani Ituri, limetokea wakati hali inatajwa kuwa ya wasiwasi katika mji wa Bunia, ambako waasi wa kundi la CODECO,wanatishia kuuteka mji wa Bunia.

Duru karibu na jeshi la serikali katika mji wa Bunia zinadokeza,kuwa majeshi yako tayari kukabiliana na waasi wa CODECO, ikiwa watajaribu kuushambulia mji wa Bunia.

Mwandishi: John Kanyunyu DW Beni