1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Ron DeSantis kutangaza nia ya kuwania urais

Daniel Gakuba
25 Mei 2023

Gavana wa jimbo la Florida nchini Marekani, Ron DeSantis anatarajiwa kutangaza nia yake ya kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican, katika uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao wa 2024.

https://p.dw.com/p/4Rm1r
Gouverneur Florida Ron DeSantis
Ron Desantis, yuko tayari kujitosa katika kinyang'anyiro cha kugombea urais wa Marekani kwa tiketi cha chama cha RepublicanPicha: Wilfredo Lee/AP/picture alliance

Nia ya Ron DeSantis ya kuwania urais ambayo kutangazwa kwake kumekuwa kukisubiriwa kwa muda mrefu, itabainishwa kupitia mahojiano ya mtandaoni, ambayo atayafanya na mfanyabiashara tajiri Elon Musk kupitia mtandao wa Twitter, yapata saa 12 jioni majira ya mashariki mwa Marekani, ambayo ni sawa na saa saba usiku leo Afrika Mashariki. Elon Musk ambaye ni mmiliki wa mtandao wa Twitter amethibitisha kuwa atazungumza na DeSantis.

Soma zaidi: DeSantis kutangaza nia ya kuwania urais Marekani

''Ndio, nitakuwa na mahojiano na Ron DeSantis ambaye atatoa tangazo kubwa. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa jambo kama hilo kufanyika mubashara kwa njia ya mtandao, maswali yakitolewa na kujibiwa moja kwa moja, bila kusoma kwenye karatasi,'' amesema Musk.

USA | Florida | Don't say gay Bill | Protest
Ron Desantis ni mpinzani mkubwa wa masuala ya ushogaPicha: Martha Asencio-Rhine/AP Photo/picture alliance

Utitiri wa wagombea wa Republican, nani atapita?

Baada ya mahojiano hayo ambayo yatakuwa ya sauti tu bila vidio, De Santis mwenye umri wa miaka 44 atafanya mahojiano na vituo mbali mbali vya televisheni za kihafidhina, kikiwemo kile cha Fox News, katika muda wa jioni wenye watazamaji wengi.

Kwa tangazo hilo, Ron De Santis atajiunga na utitiri wa wanasiasa wa Republican ambao tayari wametia nia ya kuwania tiketi ya chama hicho, na wale ambao inajulikana watajitangaza baadaye.

Soma zaidi: Joe Biden atangaza kuwania muhula wa pili wa urais

Miongoni mwa hao, ni rais wa zamani mwenye ushawishi mkubwa, Donald Trump, aliyekuwa makamu wake, Mike Pence, balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley, na Seneta wa South Carolina, Tim Scott.

DeSantis anatazamwa na wachambuzi kama mwanasiasa mwenye msimamo mkali zaidi wa kihafidhina, mwenye histroria ya upambanaji dhidi ya sera za kiliberali.

Trump wegen sexuellen Übergriffs zu Geldstrafe verurteilt
Kwa kushtukia upinzani mkali wa DeSantis, Donald Trump tayari ameanza kumpiga vijembe Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance

Mhafidhina mwenye mitazamo iliyopitiliza

Katika jimbo lake la Florida amesimamia upitishwaji wa sheria kali za kihafidhina, zikiwemo zinazopiga marufuku kuzungumzia masuala ya ushoga katika shule za umma jimboni humo.

Mnamo majira haya ya machipuko alisaini sheria inayozuia uavyaji wa mimba tangu ile ya wiki sita, muda ambao wanaharakati wanasema wanawake wengi wanakuwa hawajagundua kuwa wanao ujauzito.

Soma zaidi: Trump ajitetea, adai Wademocrat waihujumu azma yake ya urais

Mpinzani mkuu wa Ron DeSantis ndani ya chama cha Republican, Donald Trump amekuwa akifanya vita vya maneno dhidi yake kwa zaidi ya mwezi mzima, na kupitia mitandao ya kijamii amesema DeSantis hawezi kushinda uteuzi wa chama hicho, wala urais wa Marekani kwa sababu ya historia ya kura zake bungeni dhidi ya mipango ya bima ya afya kwa wote.

Trump amesema, ''DeSantis anahitaji kupandikizwa viungo vya kuwa na haiba, na nijuavyo mimi madaktari hawawezi kumpatia huduma hiyo mtu huyu asiye na shukrani.'' 

 

Vyanzo: ape,rtre