Mamia washikiliwa Uturuki | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Ankara

Mamia washikiliwa Uturuki

Vyombo vya habari vya nchini Uturuki vimeripoti kukamatwa kwa zaidi ya watu 100 nchini humo mapema Jumatatu hii wakati jeshi la polisi likiendeleza msako dhidi ya wanaounga mkono chama cha upinzani cha Kikurdi cha HDP

Hata hivyo ripoti zilizotolewa hazikueleza iwapo watu waliokamatwa walihusika na matukio ya mashambulizi ya mabomu yaliyotokea jumamosi iliyopita na kusababisha vifo vya watu 38 na wengine 155 kujeruhiwa. 

Kulingana na taarifa za kituo cha habari cha serikali, takriban watu 37 ambao ni wanachama wa chama cha upinzani cha Kikurdi, HDP walikamatwa na kutiwa kizuizini katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara. Kituo cha televisheni cha TRT pia kimeripoti matukio hayo ya kukamatwa, na kuarifu kuwa watu 58 waliotiwa kizuizini walikamatwa katika mji wa Pwani wa Mersin na 51 kutoka mji wa Sanliurfa uliopo KusiniMashariki.    

Rais Recep Tayipp Erdogan na mamlaka nyingine za nchini humo zimekituhumu chama hicho cha HDP kwa kuwa na mahusiano na chama cha wafanyakazi cha PKK, kilichopigwa marufuku. 

Serikali ya Uturuki imekuwa katika mvutano mkali na chama cha HDP tangu kufanyika kwa mapinduzi yaliyoshindwa mnamo mwezi Julai na kuwakamata baadhi ya viongozi wa kitaifa na maafisa wa ngazi za chini wa chama hicho, ingawa hakikuwa na mahusiano yoyote na jaribio hilo la mapinduzi, na wanachama wake wakisisitiza kutokuwa na mahusiano na PKK, chama ambacho kimejiingiza kwenye mapigano dhidi ya serikali kwa miaka mingi

Türkei Istanbul nach den Anschlägen (Reuters/M. Sezer)

Rais Recep Tayipp Erdogan ameahidi kukabiliana na ugaidi hadi mwisho

.

Rais Tayipp Erdogan mara baada ya kutokea kwa mashambulizi hayo amesema atahakikisha nchi yake inakabiliana na ugaidi hadi pale watakapoona wako salama, na kwamba hawatajishusha na kuwaachia maaduni kuendeleza mashambulizi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Jana alituma salamu za pole kwa rais wa Uturuki Tayipp Erdogan kufuatia mashambulizi hayo, huku kwa pamoja wakiapa kuboresha mikakati ya kukabiliana na ugaidi. Aidha Kansela Merkel kwenye taarifa yake iliyosomwa na msemaji wake Ulrike Demmer amesema bado kuna mengi yanayohitajika kufanyika katika kukabiliana na ugaidi.

Rais wa shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck naye ameeleza kushtushwa na mashambulizi hayo ya Uturuki. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank-Walter Stainmeier amesema, wanalaani vikali mashambulizi haya ya kigaidi na kwa pamoja wanashirikiana na Uturuki kuomboleza wahanga wa mashambulizi hayo.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Saumu Yusuf.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com