Makubaliano ya Serikali ya Muungano yafikiwa Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Makubaliano ya Serikali ya Muungano yafikiwa Ujerumani

Kansela Angela Merkel na muungano wa vyama vyake vya kihafidhina vya CDU, na CSU, wamekamilisha mkataba wa kuunda serikali ya muungano pamoja na SPD miezi miwili baada ya uchaguzi mkuu.

Kutoka kushoto ni mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel,Sigmar Gabriel wa SPd na Horst Seehofer wa chama cha CSU

Kutoka kushoto ni mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel,Sigmar Gabriel wa SPd na Horst Seehofer wa chama cha CSU

Makubaliano hayo ya kurasa 170 yaliyotangazwa leo alfajiri baada ya majadiliano yaliyodumu zaidi ya saa 17 yatamuwezesha kansela Angela Merkel kuunda serikali yake ya tatu kabla ya siku kuu za Krismasi. Kabla ya hapo lakini wanachama zaidi ya laki nne na 70 elfu wa SPD watabidi watamke kama wanayakubali au la.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa majadiliano yao katibu mkuu wa chama cha SPD, Andrea Nahles, amechambua mada zilizokubaliwa akisema:"Ni pamoja na kiwango cha chini cha mishahara, Euro 8 na nusu kwa saa moja ya kazi kuanzia mwaka 2015, bila ya shaka umri wa mtu kuweza kustaafu, fedha zaidi kwa serikali za miji na katika sekta ya elimu na tumefanikiwa kweli kwa namna ambayo tunaweza kusema hakuna mtoto aliyezaliwa na kukulia huku atakayelazimishwa tena kuchagua uraia. Haya ni baadhi ya matokeo ya mazungumzo ambayo tunahisi tunaweza kuyafikisha mbele ya wafuasi wetu na tunaweza kuwashauri waseme ndio wameyakubali."

Makubaliano ya Maana kwa Ujerumani

Große Koalition CDU und SPD einigen sich 27. Nov. 2013 Dobrindt und Gröhe

Makatibu wakuu wa vyama ndugu vya CDU na CSU,Alexander Dobrindt (kulia) na Hermann Gröhe

Hata wawakilishi wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU wameridhika na makubaliano yaliyofikiwa. "Makubaliano yaliyofikiwa ni ya maana kwa nchi yetu," amesema katibu mkuu wa chama cha Christian Democratic Union, Hermann Gröhe, akihoji makubaliano yana muhuri wa kihafidhina; "hakuna kodi ya ziada wala mikopo ya ziada," amesema.

Pindi wanachama wa SPD wakiunga mkono mkataba wa kuunda serikali kuu ya muungano Desemba 14, Angela Merkel atachaguliwa na wabunge Desemba 17 ijayo kuiongoza serikali ya muungano wa vyama vikuu kwa muhula wa tatu wa miaka minne.

Nani atakabidhiwa Wizara Gani?

Große Koalition CDU und SPD einigen sich 27. Nov. 2013 Kraft und Steinmeier

Frank Walter Steinmeier na waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia bibi Hannelore Kraft.

Wakuu wa vyama vyote hivyo vya kisiasa wanatarajiwa baadaye hii leo kuitisha mkutano na waandishi habari kuzungumzia makubaliano yaliyofikiwa. Suala la nani atakabidhiwa wizara gani litajibiwa pengine baadaye.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com