1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Majaji Tanzania waonywa kuhusu upendeleo na uzembe

Admin.WagnerD2 Februari 2026

Nchini Tanzania, majaji na mahakimu wametakiwa kutokutumia dhana ya uhuru wa mahakama kama kisingizio cha kuficha uzembe, upendeleo au maamuzi yasiyo ya haki wanaposhughulikia kesi mbalimbali.

https://p.dw.com/p/57w0q
Makamu wa Rais wa Tanzania Emanuel Nchimbi
Makamu wa Rais wa Tanzania Emanuel NchimbiPicha: Office of the Deputy President of Tanzania

Mwito huo umetolewa katika  maadhimisho ya siku ya sheria nchini Tanzania. 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Tanzania Emanuel Nchimbi alipokuwa akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa maadhimisho ya sherehe ya siku ya sheria nchini Tanzania.

Katika maadhimisho hayo, yalio hudhuriwa na viongozi wa sekta ya sheria imesisitizwa kuwa uhuru wa mahakama ni msingi muhimu wa haki, lakini haupaswi kugeuzwa ngao ya kujilinda dhidi ya udhaifu wa kiutendaji.

Aliongeza kuwa ipo haja ya watendaji wa mahakama kuhakikisha wanatoa maamuzi yanayoendana na misingi ya sheria, ushahidi na haki, bila kuathiriwa na maslahi binafsi au ushawishi wa nje.

Aidha, ilisisitizwa kuwa jamii inatarajia kuona majaji na mahakimu wakisimamia kwa uadilifu mchakato mzima wa utoaji haki, hususan katika kipindi ambacho mahitaji ya uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma yanaendelea kuongezeka.

Makamu wa rais alionya kuwa vitendo vya upendeleo, ucheleweshaji usio na sababu na maamuzi yenye kubeba hisia binafsi vinahatarisha imani ya wananchi katika mfumo wa haki.

Aidha Nchimbi amesema kuwa mahakama inao wajibu wa kulinda utawala wa sheria, utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha watanzania wote kwa usawa.

TLS: Juhudi za dhati zifanyike kuleta 'umoja wa kitaifa'

Kwa upande wake rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika TLS, Boniphace Mwabukusi, akizungumza katika sherehe hizo za siku ya sheria nchini Tanzania zilizofanyika jijini Dodoma, amesema kuwa chama cha mawakili Tanganyika kinatambua changamoto kubwa iliyoipata Tanzania kutokana na yaliyojiri kabla na mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana na kwamba lazima kuwe na hatua za muhimu na uwajibikaji ili kurejesha imani na matumaini ya wananchi katika taifa lao.

Tanzania: Ushahidi mpya juu ya mauaji ya Oktoba 2025

Tanzania inaadhimisha siku ya sheria huku kukiwa na hali ya majonzi kutokana na matukio yaliyotokea mnamo Oktoba 29 mwaka jana kabla na mara baada ya uchaguzi ikiwemo vifo vya watu na uharibifu wa mali. Tayari Rais Samia ameunda Tume kuchunguza matukio hayo.