1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKimataifa

Amnesty: Walionyongwa wafika idadi ya juu katika miaka 44

18 Mei 2026

Idadi ya watu walionyongwa duniani kote mwaka 2025 iliongezeka na kufikia idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa na Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International tangu 1981.

https://p.dw.com/p/5Dt9g
Waandamanaji walikusanyika nje ya Ubalozi wa Iran mjini Berlin kumuunga mkono kiongozi wa upinzani wa Iran Reza Pahlavi
Amnesty International imesema jumla ya watu 2,707 walinyongwa katika nchi 17 kote ulimwenguniPicha: Michael Kuenne/PRESSCOV/Sipa USA/picture alliance

Mkuu wa Amnesty Agnes Callamard amesema katika taarifa iliyochapishwa leo kuwa ongezeko hili la kutisha katika matumizi ya adhabu ya kifo linatokana na kundi dogo la mataifa yaliyotengwa na yaliyo tayari kutekeleza hukumu ya kifo kwa gharama yoyote ile, licha ya mwelekeo unaoendelea wa kimataifa wa kukomesha adhabu hiyo. Callamard alizitaja China, Iran, Korea Kaskazini, Saudi Arabia, Yemen, Kuwait, Singapore na Marekani, akisema kwamba "kundi hili la walio wachache wasio na haya linatumia adhabu ya kifo kama silaha ili kusababisha hofu, kuangamiza upinzani na kuonyesha nguvu ambazo taasisi za serikali zinazo dhidi ya watu wasiojiweza na jamii zilizotengwa." Amnesty ilisema ongezeko hilo, ambalo ililielezea kama "la kushangaza," lilitokana na serikali chache zilizoazimia kutawala kwa hofu.

Mashirika ya haki za binaadamu pamoja na Amnesty yamebainisha kuwa Iran inaongeza tena matumizi yake ya adhabu ya kifo katika mwaka 2026 baada ya maandamano ya Januari na vita dhidi ya Israel na Marekani. Kumekuwa na matukio ya watu kunyongwa kwa mashtaka yanayohusiana na maandamano hayo na uanachama wa makundi yaliyopigwa marufuku.

Maandamano ya kupinga adhabu ya kifo nchini Iran, yaliyofanyika mjini Cologne, Ujerumani
Amnesty imesema karibu watu 2,159 walinyongwa nchini Iran, zaidi ya mara mbili ya idadi ya 2024.Picha: Christoph Hardt/Future Image/IMAGO

Amnesty imesema idadi jumla inayojulikana ya kunyongwa watu 2,159 nchini Iran mwaka wa 2025 – ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko ile iliyochapishwa na shirika lisilo la kiserikali la haki za binadamu la Iran lenye makao yake makuu Norway mapema mwaka huu -- "ilikuwa idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu 1981" nchini humo. Pia ilikuwa ndio idadi kubwa zaidi duniani tangu mwaka huo.

Lakini pia ilibainisha kuwa China ilikuwa "mtekelezaji mkuu wa adhabu ya kifo duniani," ikidai kwamba maelfu ya watu walinyongwa huko katika mwaka wa 2025.

Nchi zingine zilizoangaziwa ni Saudi Arabia ikiwa na karibu watu 356, hasa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, Marekani ikiwa na watu 47 walionyongwa na Misri ikiwa na watu 23.

Ripoti hiyo imesema kuwa katika mwaka wa 2025, idadi ya walionyongwa ilipanda kwa asilimia 78baada ya karibu visa 1,518 kurekodiwa katika mwaka wa 2024.

Chumba cha kutekeleza adhabu ya kifo katika Gereza la Jimbo la Oklahoma katika mji wa McAlester
Marekani ilikuwa nchi pekee katika mabara ya Amerika kunyonga watu mwaka 2025Picha: Sue Ogrocki/AP Photo/picture alliance

Kwingineko, Amnesty ilibainisha kwamba Burkina Faso ilipitisha rasimu ya muswada ambayo ilijumuisha kurejesha adhabu ya kifo kwa makosa kama vile "uhaini," "ugaidi," na "vitendo vya ujasusi," huku mamlaka nchini Chad ikiwa imeunda tume ya kupitia masuala yanayohusiana na adhabu ya kifo, ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwake.

Lakini shirika hilo pia iliona maendeleo katika majaribio ya kukomesha sheria hiyo. Ilipoanzisha kampeni yake dhidi ya adhabu ya kifo mwaka wa 1977, ni nchi 16 pekee ndizo zilizoifuta. "Leo hii, idadi hiyo imeongezeka hadi 113 - zaidi ya nusu ya nchi zote duniani, huku zaidi ya theluthi mbili zikiipinga katika sheria au matumizi yake"

Callamard amesema huku haki za binadamu zikiwa hatarini kote ulimwenguni, mamilioni ya watu wanaendelea kupigana dhidi ya adhabu ya kifo kila mwaka katika dhihirisho kubwa la ubinadamu wetu wa Pamoja.

DPA, AFP