1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahujaji elfu 60 wakusanyika Mlima Arafat

Sudi Mnette
19 Julai 2021

Mahujaji elfu 60 wamekusanyika katika eneo la Mlima Arafat, nchini Saudi Arabia ikiwa ni sehemu muhimu na ya mwisho kabla ya kuhitimisha ibada ya Hijja, huku kukiwa na masharti makali ya kukabiliana na virusi vya corona 

https://p.dw.com/p/3wgTi
Saudi-Arabien Mekka | Erste Pilger nach Coronasperrung
Picha: AFP/Getty Images

Ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona, leo hii pia mahujaji watasimama kwenye Mlima wa Arafat kwa siku nzima, mahala ambako Mtume Muhammad (S.A.W.) alitoa khutba yake ya mwisho karne 14 zilizopita. Baadae mahujaji hao watarudi Menna kwa utaratibu wa kumpiga mawe Shetani, ikiwa ni kuanza kwa Siku kuu ya Idd el Adha ama Idd el Hajj.

Tofauti na miaka iliyopita, ambako eneo hilo la mlima kulishuhudiwa uwepo wa watu zaidi ya milioni 2.5, safari hii kutokana na serikali ya Saudi Arabia kuchagua idadi maalumu ambapo mlima umeonekana kuwa kama mtupu. Hakuna kabisa ummati mkubwa wa watu ambao kwa kawaida huonekana ukishuka juu yake.

Hali nzuri kwa mahujaji wote 60,000.

Mekka-Wallfahrt - muslimische Pilgerreise - Steinigung des Teufels in Mina
Mahujaji wakiwa Mina, Saudi ArabiaPicha: picture-alliance/dpa/M. Biber

Mmoja kati ya waliochaguliwa kushirikia ibada hiyo, Selma Mohammed Hegazi mwenye umri wa miaka 45 aliliambia shirika la Habari la Ufaransa AFP kwamba, kubahatika kwake kuwa miongoni mwa wachache katika ibada hiyo ni ishara kwamba Mungu anawasamehe, na ibada yao atairidhia. Nasser Al-Qaisi kutoka hujaji kutoka Jordan ane aliiongeza zaidi"Hijja imekuwa nzuri sana, maandalizi mazuri,mazingira ya kuzingatia afya na salama. Kumekuwa na nafasi kati mahujaji na huduma zote zinapatikana."

Huko huko Saudi Arabia serikali imetangaza kuanzia Agosti 9 wananchi wake hawataruhusiwa kusafiri nje ya taifa hilo pasipo kukamilisha chanjo zote mbili za Covid-19. Uamuzi huo unatokana na uwepo wa mawimbi mapya ya virusi, kubadilika kwa virusi na ufanisi mdogo wa chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Uingereza imeyaondoa masharti ya kukabiliana na virusi vya corona kwa umma.

Katika hatua nyingine Uingereza leo hii imeyaondoa masharti ya kukabiliana na janga la virusi vya corona katika maisha ya kila siku ya watu wa taifa hilo hatua ambayo imekosolewa vikali na wanasayansi pamoja na wanasiasa, wakisema ni kama hatari ya kulipeleka taifa hilo kusikojulikana.

Vilabu vya usiku na majumba ya michezo yameruhusiwa kufanya shughuli zake kama kawaida, wakati sheria iliyokuwa ikiwalazimisha watu kuvaa barakoa katika maeneo ya wazi na kufanya kazi nyumbani vyote vimewekwa kando kabisa. Lakini waziri mkuu ambae hivi karibuni alijitenga kutokana na kupata maambukizi amewataka wananchi kuchukua tahadhari.

Na wakati huu ulimwengu ukijiandaa na mashindano ya Olimpiki ya Tokyo Japan yatakayoaznza Julai 23 hadi Agosti 8, mchezaji wa mpira wa wavu wa Jamhuri ya Czech, amekutwa na virusi vya corona alipowasili katika kijiji cha michezo hiyo.

Vyanzo: AFP/RTR