Mahakama ya Ulaya yaihusisha Urusi kwenye mauaji ya jasusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

URUSI

Mahakama ya Ulaya yaihusisha Urusi kwenye mauaji ya jasusi

Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya imeibebesha hatia Urusi kwa mauaji ya aliyekuwa jasusi wake, Alexander Litvinenko, yaliyofanyika mwaka 2006 jijini London, huku Urusi yenyewe ikiita hukumu huo kuwa ya kisiasa.

Uamuzi wa leo (Jumanne, 21 Septemba) wa mahakama hiyo ya juu kabisa barani Ulaya umetokana na shauri lililofunguliwa na kizuka wa Litvinenko, Marina, ambaye aliitaka mahakama hiyo kuchunguza na kumtangaza muhusika mkuu wa mauaji ya mumewe. 

Mahakama hiyo imesema imeweza kuthibitisha pasina shaka kwamba mauaji hayo yalifanywa na raia wawili wa Kirusi, Andrei Lugovoi na Dmitry Kovtun. 

Majasusi hao wawili walisafiri kwenda kwenye mji mkuu wa Uingereza, London, kwa dhamira ya kumuuwa jasusi mwenzao wa zamani, imesema mahakama hiyo katika hukumu yake. 

"Operesheni hiyo changamano ilipangwa ikihusisha ununuwaji wa sumu kali na adimu sana kupatikana, mipango ya usafiri ya wawili hawa, na majaribio kadhaa na endelevu kuhusu sumu hiyo, yote yanaashiria kwamba Bwana Litvinenko alikuwa ndiye mlengwa." Ilisema hukumu hiyo.

London Marina Litwinenko Witwe von Ex-Spion Alexander Litwinenko

Marina, kizuka wa Alexander Litvinenko.

Lugovoi, ambaye sasa ni mbunge nchini Urusi, na mfanyabiashara Kovtun walitambuliwa na polisi nchini Uingereza kama washukiwa wakuu baada ya wote wawili kukutana na Litvinenko katika hoteli moja iliyopo katikati ya London.

Liitvinenko alikufa baada ya kunywa chai iliyochanganywa na mionzi ya sumu aina ya Polonium 210 kwenye hoteli hiyo, katika mkasa ambao tangu hapo umeyaathiri sana mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Lakini majaribio ya kuwasafirisha kutoka Urusi na kuwaleta Uingereza kukabiliana na kesi dhidi yao yalishindikana, na wote wamekanusha mashitaka hayo, huku Lugovoi akidai pia kutumia kinga yake ya kibunge.

Mfululizo wa majaribio ya mauaji

Kabla ya kifo chake, Litvinenko alitoa ujumbe akimshutumu Rais Vladimir Putin kwa kumtilia sumu. Wapinzani wa Putin wanayachukulia mauaji hayo kuwa ya kwanza kwenye orodha refu ya hujuma za Kremlin dhidi ya wakosoaji wake.

 Alexander Litvinenko Ex-KGB Agent Russland

Alexander Litvinenko (kulia) akiwa na mwenzake kabla ya kufariki dunia mwake 1998.

Hata hivyo, msemaji wa Putin, Dmitry Peskov ameutupilia mbali uamuzi wa leo wa Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya, akisema kwamba hauna mashiko yoyote ya maana.

"Bado hakuna matokeo ya uchunguzi, kwa hivyo kutoa kauli kama hizo hakuna mashiko yoyote. Hatuko tayari kukubaliana na uamuzi huu." Alisema Peskov.

Hayo yakijiri, polisi nchini Uingereza imetangaza hivi punde kwamba ina ushahidi wa kutosha wa kumshitaki raia wa tatu wa Kirusi kwa kumshambulia kwa sumu aina ya Novichok, jasusi mwengine wa zamani, Sergei Skripal, na binti yake, Yulia, katika mji wa Salisbury mnamo mwaka 2018.

Wapelelezi wa kikosi cha kupambana na ugaidi walisema waendesha mashitaka wamepitia upya ushahidi dhidi ya mtu aliyetambuliwa kwa jina la Sergey Fedotov kwa ajili ya kumfungulia mashitaka ya mauaji, jaribio la mauaji, kusababisha madhara mwilini, na kumiliki na kutumia silaha ya kemikali. 

Kama ilivyokuwa kwa Litvinenko, jasusi huyo wa zamani wa KGB naye alimtuhumu moja kwa moja Rais Putin kwa mashambulizi hayo, katika barua iliyosomwa hadharani baada ya kifo chake.