Magufuli asema corona haitazuwia uchaguzi mkuu Tanzania | Matukio ya Afrika | DW | 26.03.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Magufuli asema corona haitazuwia uchaguzi mkuu Tanzania

Rais wa Tanzania John Magufuli amesema serikali yake itafanya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama kawaida licha ya wengi kudhani huenda ukahairishwa kutokana na janga la Covid-19.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Alhamisi wakati akipokea ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali pamoja na ripoti ya taasisi ya kupambana na rushwa nchini humo TAKUKURU katika ikulu ya Chamwino mjini Dodoma.

Kauli hiyo imefuatia ripoti za baadhi ya vyombo vya habari nchini humo juu ya kufanyika kwa vikao vya baraza la madiwani katika halmashauri kadhaa, hatua ambayo imemlazimu Rais Magufuli kutolea ufafanuzi kuwa kuna umuhimu wa kazi na lazima kuendelea, ikiwemo vikao vya madiwani, bunge pamoja na vikao mbalimbali vya kiutendaji kwa maslahi mapana ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Deni la taifa lafikia trilioni 53

Ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali imeonyesha kuwa deni la taifa limeendelea kukua hadi kufikia  shilingi trilioni 53.11 ambapo deni la ndani ni trilioni 14.86 na deni la nje likiwa trilioni 38.24.

Kiasi hicho kinawakilisha ongezeko la asilimia 4 kutoka mwaka 2018, lililosababishwa na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania. Wachambuzi wanasema hata hivyo kuwa deni hilo linaendelea kuhimilika.

Tansania Dar es Salaam Vereidigung Controller Auditor General CAG

Mkguzi mkuu wa hesabu za serikali Charles Kichere, kulia alipoapishwa katika wadhifa huo Novemba 3, 2019. Kichere amewasilisha ripoti yake ya kwanza kwa rais Magufuli, Machi 26, 2020.

Mkaguzi mkuu wa hesabu za serilikali Charles Kichele ikiwa ni mara ya kwanza kuwasilisha ripoti hiyo tangu kuteuliwa katika wadhifa huo, amemwambia rais Magufuli kuwa walikagua pia katika vyama vya siasa.

Amesema ukaguzi wa Chama cha Wanachi CUF, umeonyesha kuwa kiasi cha shilingi milioni mia tatu kilihamishwa na kupelekwa kwenye akaunti binafsi ya mwanachama huku chama tawala CCM kikifanya malipo yasiyo na tija kiasi cha milioni sitini bila kuwa na utaratibu maalum.

Juhudi za kudhibiti rushwa zaanza kuonekana

Hali inaonekana kuimarika katika kudhibiti masuala ya rushwa katika taifa hilo ambapo mashirika ya kimataifa ikiwemo Transparency International ikilitaja taifa hilo kushika nafasi ya 98 kati ya mataifa 183 kwa mwaka 2019 ikitoka nafasi ya 119 kabla ya serikali ya awamu ya tano kushika hatamu ya uongozi mwaka 2015.

Katika ukanda wa maziwa makuu Tanzania imeendelea kushika nafasi ya pili katika udhibiti, amesema aliyekuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa Takukuru brigedia jenerali John Mbungo.

Kwa mujibu wa taasisi ya kupambana na rushwa kiasi cha shilingi bilioni 8.8 zimeokolewa katika harakati za kudhibiti vitendo vya rushwa vyenye matokeo ya kuhujumu uchumi wa taifa hilo unaokuwa kwa wastani wa asilimia saba.

Ni mafanikio yanayoonesha kumridhisha rais John Magufuli, hivyo kumpandisha wadhifa brigedia jenerali John Mbungo kuwa mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo nyeti katika kukabiliana na masuala ya rushwa nchini humo.