Macron afanya mazungumzo na Putin | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Macron afanya mazungumzo na Putin

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekutana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin nje kidogo ya Paris jioni ya Jumatatu(29.05.2017) na wawili hao wamezungumza juu ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili.

Macron ambaye aliingia madarakani wiki mbili zilizopita amesema mazungumzo yake na Urusi ni muhimu sana katika kushughulikia migogoro kadhaa ya kimataifa. Hata hivyo, mahusiano yamekuwa ya kutoaminiana kwasababu Ufaransa  na Urusi zinaunga mkono pande tofauti katika vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria na pia kupingana juu ya mgogoro wa Ukraine.

Akiwa amemaliza mazungumzo na viongozi wenzake wa mataifa ya magharibi katika mkutano wa Jumuiya ya kujihami NATO mjini Brussels na ule wa nchi saba G7 zilizoendelea duniani mjini Sicily, Macron amemkaribisha rais wa Urusi katika kasri la karne ya 17 la Ikulu ya Versailles nje kidogo ya Paris.

Frankreich - Paris - Vladimir Putin trifft Emmanuel Macron (Getty Images/AFP/G. van der Hasselt)

Macron akiwa na rais Putin Versailles

Marais hao watahudhuria ufunguzi wa kumbukumbu ya miaka 300 ya ziara ya Mfalme Peter wa Urusi mjini Paris. Rais huyo mwenye miaka 39 alimpokea mgeni wake Putin na kisha wakasalimiana kwa kupeana mikono na kuingia ndani ya Ikulu kwa mazungumzo.

Balozi wa Urusi kwa Ufaransa Alexander Orlov amesema anamatumaini mkutano huo utasaidia kuyaimarisha mahusiano yaliozorota  baina ya Putin na mtangulizi wa Macron, Francois hollande. "Ninadhani kuanza kuondoa hali ya kutoaminiana ambayo imekuwepo katika mika ya hivi karibuni ni muhimu sana na ninafikiria katika masaa machache yajayo tutakuwa na msingi mzuri", alisema balozi huyo.

Wakati akiwa mjini Sicily, Macron alisema ni muhimu kufanya mazungumzo na Urusi kwa kuwa yapo mambo mengi ya kimataifa ambayo hayawezi kutatuliwa pasipo kubadilishana na Urusi. Katika mkutano huo viongozi wa mataifa ya Magharibi walikubaliana kuzingatia hatua mpya ikiwa hali ya Ukraine haitaimarika.

Mahusiano baina ya Paris na Moscow yalikuwa yametetereka wakati wa utawala wa rais Francois Hollande. Putin mwenye miaka 64, alifuta ziara yake ya Paris iliyokuwa imepangwa mwezi Oktoba baada ya Hollande kuituhumu Urusi kwa makosa ya uhalifu wa vita nchini Syria na kukataa kumtandikia zulia jekundu.

Frankreich - Paris - Vladimir Putin trifft Emmanuel Macron (Getty Images/AFP/S. de Sakutin)

Putin akipunga mkono mara baada ya kuwasili

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Ufaransa, timu ya Macron ilidai kwamba Urusi ilijaribu kudukua taarifa za mgombea wao na wakati mmoja iliwanyima vitambulisho waandishi wa vyombo vya habari vya taifa vya Urusi Sputnik na shirika la habari la Urusi RT na kusema vilikuwa vikieneza propaganda za Urusi na habari za uwongo.

Siku mbili kabla ya uchaguzi wa Mei 7, timu ya Macron ilidai pia kwamba maelfu ya barua pepe za kampeni zilidukuliwa na kuvujishwa mtandaoni ambapo mchambuzi mmoja wa New York alisema hiyo inawezekana ilitoka kwa kundi lenye mahusiano na ujasusi wa kijeshi wa Urusi.

Putin pia atakitembelea kituo cha Urusi cha utamaduni na kiroho cha madhehebu ya kikristo ya Orthodox ambacho alikuwa akifunguwe mwezi Oktoba kabla ya kuahirisha  ziara yake .

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com