Lebanon kuchagua bunge jipya Jumapili | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Lebanon kuchagua bunge jipya Jumapili

Taifa la Lebanon litafanya uchaguzi wa wabunge Jumapili. Uchaguzi huo utakuwa wa 14 tangu taifa hilo lijinyakulie uhuru wake mwaka 1943.Lebanon inachukuliwa kuwa taifa la kiliberali, lakini dini inasalia kuwa muhimu.

Lakini huu uchaguzi unafanyika huku taifa hilo likiwa limekumbwa na mzozo wa kisiasa wa muda mrefu, uchumi uliozorota na kugawanyika kutokana na mzozo unaoendelea nchi jirani ya Syria, ambayo imekuwa na ushawishi mkubwa kwenye taifa hilo dogo la Mashariki ya Kati.

Lebanon yenye bendera ya mti wa mkangazi ni moja ya mataifa madogo kwenye eneo la Mashariki ya Kati likiwa na eneo lenye mraba wa yumkini kilomita 10,000. Magharibi inapakana na bahari ya Mediterranea, na upande mwingine inapakana na Syria na Israel.

 Lebanon ni taifa la kiliberali    

Licha ya udogo wake, hata hivyo, Lebanon ni taifa lenye mfumo wa kiliberali katika ukanda ambao unaokena kuwa wa kihifadhina. Hata hivyo, suala la dini linasalia kuwa muhimu. Utawala wake unaongozwa kwa maafikiano kutoka kwa dini 18 zinazojenga taifa hilo.

Lebanon ni jamhuri inayoongozwa na bunge ikiwa na wabunge 128 - ambao wamegawanyika, baadhi yao ni Wakristo huku wengine wakiwa Waislamu wa madhehebu mbili kubwa, Shia na Sunni.

Rais wakipiga kura Lebanon

Rais wakipiga kura Lebanon

Kwa kuzingatia maafikaino ya kitaifa ambayo yalifanyika taifa hilo lilipojinyakulia uhuru, rais lazima awe Mkristo, waziri mkuu Muislamu wa Sunni na spika wa bunge awe Shia.

Kuzuka kwa vita nchini Syria mwaka 2011, ambayo utawala wake ulikalia Lebanon kwa kipindi cha miaka 29 pamoja na vuguvugu la Washia wa Lebanon kumechangia mgawanyiko mkubwa zaidi.

Mzozo huo sasa umesambaa hadi Lebanon, huku mashambulio ya maroketi na yale ya kujitoa mhanga yakiripua mji mkuu wa Beirut na maeneo mengine, lakini taifa hilo kwa kiwango kikubwa limeviepuka vita hivyo.

Athari kubwa inayoonekana kwenye vita vya Syria nchini Lebanon ni kuiingia kwa idadi kubwa ya wakimbizi inayokadiriwa kuwa milioni 1.5, ambao sasa ni robo ya idadi ya watu katika taifa hilo.

Uchumi wa Lebanon kama mataifa mengine katika kanda hiyo umekuwa ukisambaratika kwa miaka, huku deni la taifa likifikia asilimia 150 ya jumla ya pato la taifa, kiwango cha tatu cha juu ulimwenguni nyuma ya Japan na Ugiriki.

Uchumi wake umeshuka kwa asilimia mbili

Uchumi huo uliotegemea huduma ulikuwa unakua kwa asilimia 10 kila mwaka kabla ya vita vya Syia kuanza, lakini sasa ukuaji huo umeshuka kwa asilimia mbili pekee.

Aliyekuwa waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri

Aliyekuwa waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri

Pengo kati ya matajiri na masikini limeongezeka, idadi ya watu wasio na ajira imeongezeka maradufu kati ya mwaka 2011 na 2014 na kufikia asilimia 20, serikali haiwezi bado kuwapa wakazi wake maji na umeme hata katika mji mkuu wa Beirut.

Mwaka 1947, Lebanon iliandaa uchaguzi na wabunge 55 wakachaguliwa. Kwa kuzingatia mwafaka wa kugawana mamlaka kati ya dini za Waislamu na Wakristo, chombo hicho kiliongozwa na kima cha Wakristo sita kwa kila Waislamu watano.

Uchaguzi uliofanyika mwaka 1992 ulikuwa wa kwanza kufanyika tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo uchaguzi wa mwisho uliandaliwa mwaka 1972.

Ni mara ya kwanza kwa wapiga kura kuwachagua wabunge 128 baada ya makubaliano ambayo yalimaliza vita na kupanua chombo hicho kati ya Waislamu na Wakristo.

Mwezi Juni mwaka 2017 vyama hasimu vilikubaliana kuhusu sheria mpya za uchaguzi baada ya mazungumzo ya muda mrefu.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Afp, Ape

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com