Kura zaanza kuhesabiwa Ethiopia | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kura zaanza kuhesabiwa Ethiopia

Zoezi la kuhesabu kura limeanza nchini Ethiopia baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika jana, ukiwa ni wa kwanza kabisa tangu kifo cha waziri mkuu Meles Zenawi. Uchaguzi unaendelea leo kuwaruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu.

Maafisa wakiendelea kuhesabu kura

Maafisa wakiendelea kuhesabu kura

Jana Jumapili, wananchi wa Ethiopia walipiga kura katika uchaguzi huo wa wabunge, ambao chama tawala cha Waziri Mkuu, Hailemariam Desalegn cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front-EPRDF, kinatarajiwa kupata ushindi mkubwa na kuendeleza utawala wake.

Chama hicho ambacho kimetawala kwa miaka 24, kwa sasa kina jumla ya viti 546 katika bunge la nchi hiyo lenye viti 547. Karibu asilimia 80 ya wapiga kura milioni 37 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo ambao wengi wanatabiri matokeo yake yanajulikana, katika nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni 94.

Wapigakura wa upinzani jana walidai kuwepo unyanyasaji na hata vurugu katika baadhi ya vituo vya kupigia kura. Baadhi ya viongozi wa upinzani wamesema wanachama wao walipigwa na kubugudhiwa wakati wa zoezi la kupiga kura.

Mwananchi wa Ethiopia akipiga kura jana

Mwananchi wa Ethiopia akipiga kura jana

Msemaji wa chama cha upinzani cha Blue, Yonathan Tesfaye, amesema wamepokea malalamiko mengi kutoka kwa waangalizi ambao walizuiwa kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi. Aidha, mgombea wa chama cha upinzani, Bekele Nagaa, amesema wawakilishi wao waliondolewa kwenye vituo vya kupigia kura.

''Wanalazimishwa kuwapigia kura EPRDF. Maafisa wa uchaguzi katika baadhi ya maeneo tayari wameondoka na viongozi wa EPRDF wamechukua jukumu la kusimamia uchaguzi na wanawachagulia wapiga kura watu wa kuwachagua kwa lazima,'' alisema Nagaa.

Serikali yasema uchaguzi umefanyika kwa amani

Hata hivyo, shirika la habari la Ethiopia, limewanukuu waangalizi wa Umoja wa Afrika wakisema kuwa uchaguzi umefanyika vizuri kama ilivyopangwa. Waziri wa Serikali anayeshughulikia masuala ya Mawasiliano ya Serikali, Shimelis Kemal, amesema zaidi ya asilimia 85 ya watu walijitokeza kupiga kura na zoezi la kupiga kura limefanyika kwa amani.

Jana jioni Bodi ya Uchaguzi ya Ethiopia ilisema wanafunzi wa vyuo vikuu watapiga kura leo baada ya uchaguzi kuongezwa muda kutokana na hitilafu zilizojitokeza baada ya kukosekana baadhi ya vifaa vya kupigia kura.

Uchaguzi huo unavishirikisha vyama 58 vya siasa na matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa baada ya wiki moja, lakini matokeo ya mwisho yatatangazwa kabla ya Juni 22. Mwaka 2010, chama tawala cha EPRDF kilishinda uchaguzi kwa asilimia 99.6, ambapo mgombea mmoja tu wa upinzani ndiye alishinda katika uchaguzi huo.

Waziri Mkuu, Hailemariam Desalegn

Waziri Mkuu, Hailemariam Desalegn

Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International, yameikosa Ethiopia kwa kuwakandamiza wanasiasa na waandishi wa habari na yamesema kwamba vyama vya siasa vimekuwa vikibugudhiwa sana wakati wa kampeni za uchaguzi.

Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn amekuwa akiiongoza Ethiopia tangu alipofariki dunia Meles Zenawi mwaka 2012, ambaye aliujenga muungano wa chama tawala kuwa wenye nguvu sana kisiasa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com