Ethiopia kuandaa uchaguzi mkuu Jumapili | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ethiopia kuandaa uchaguzi mkuu Jumapili

Ethiopa, taifa la pili lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika linafanya uchaguzi mkuu Jumapili hii, uchaguzi wa kwanza tangu kifo cha Meles Zenawi aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo aliyeongoza kwa mkono wa chuma.

Hailemariam Desalegn mwenye umri wa miaka 49 ambaye aliingia madarakani mwezi Septemba mwaka 2012 baada ya kifo cha Meles Zenawi anapigiwa upatu kurejea madarakani kama waziri mkuu wa Ethiopia katika uchaguzi huo wa Jumapili.

Zaidi ya raia milioni 36.8 nchini humo wamesajiliwa kama wapiga kura. Nchi hiyo ina idadi ya watu milioni 94. Uchaguzi huo mkuu unachukulika na jumuiya ya kimataifa kuwa kipimo kikubwa cha kutathimini kujitolea kwa taifa hilo kutanua nafasi yake ya kidemokrasia.

Serikali yashutumiwa kuwa kandamizi

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakiishutumu serikali ya Ethiopia kuwa inawakandamiza wafuasi wa vyama vya upinzani na wanahabari na inatumia sheria za kupambana na ugaidi kuwanyamazisha wakosoaji wake.

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Chama tawalwa cha Ethiopia People's Revolutionary Democratic Front EPRDF kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita na kina matumaini makubwa kitashinda katika uchaguzi huo.

Chama hicho kinasisitiza kuwa matokeo yataamuliwa na rekodi nzuri iliyo nayo kuhusiana na masuala ya kiuchumi. Taifa hilo ni miongoni mwa mataifa ya bara Afrika yanayofanya vizuri kiuchumi na yamevutia uwekezaji wa kigeni.

Msemaji wa serikali Redwan Hussein amesema kumekuwa na ufanisi mkubwa nchini humo na watu wamejionea na iwapo raia watataka serikali isalie madarakani uamuzi ni wao lakini hatarajii kuwa watapoteza viti vingi katika uchaguzi huo.

Kulingana na benki ya dunia, Ethiopia imeshuhudia ukuaji wa kiuchumi wa zaidi ya asilimia kumi kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Waziri mkuu Hailemariam amesema ana nia ya kuhakikisha mfumo wa kisiasa nchini Ethiopia unapanuka kwa kuvipa nafasi na uhuru zaidi vyama vya upinzani.

Waziri mkuu asema ataruhusu demokrasia kutanuka

Hailemariam amesema kutokuwepo kwa demokrasia ya vyama vingi nchini Ethiopia kutaifanya nchi yake kuwa kama Somalia. Licha ya hakikisho hilo kutoka kwa serikali, vyama vya upinzani vimeishutumu kwa kutumia mbinu za kiimla kuhakikisha inashinda katika uchaguzi.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Blue Party wakifanya kampeini Addis Ababa

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Blue Party wakifanya kampeini Addis Ababa

Kiongozi wa chama cha kikuu cha upinzani cha Blue Party Yilekal Getinet amesema uhuru wa kisiasa umekandamizwa na wanahabari wengi, wanaharakati wa kisiasa na viongozi wa asasi za kiraia wamefungwa jela au kulazimika kutoroka nchini humo.

Tume ya uchaguzi imetangaza wachunguzi 40,000 wa uchaguzi watatumwa katika vituo 45,795 vya kupigia kura. Wachunguzi wa kigeni wa uchaguzi ni wa kutoka kwa Umoja wa Afrika pekee iliyotuma waangalizi 59. Umoja wa Ulaya na Marekani hazikualikwa kutuma waangalizi katika uchaguzi huo.Katika uchaguzi uliopita mwaka 2010, chama tawala kilishinda viti 545 vya bunge kati ya viti 547.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri: Mohammed Khelef.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com