Kongamano la Afrika nchini Ujerumani kulenga kuimarisha uhusiano na bara Ulaya | Matukio ya Afrika | DW | 09.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kongamano la Afrika nchini Ujerumani kulenga kuimarisha uhusiano na bara Ulaya

Wanasiasa, wafanyabiashara na wawakilishi wa asasi za kiraia wanakutana Jumatano kwenye Mkutano wa kwanza wa Afrika mjini Berlin, Ujerumani

 

Katika kongamano hilo, washirika hao watajadili njia mpya za ushirikiano kati ya bara la Ulaya na Afrika. Wataalam wanahimiza kubadilishwa kwa malengo na kuzingatia ubunifu wa ajira. Waandalizi wa hafla hiyo; Mpango wa malengo ya dunia (GPI), wameandika kuwa mabara ya Ulaya na Afrika yote yameathirika pakubwa na ugonjwa wa COVID-19, lakini wakaongeza kuwa janga hilo pia linawakilisha fursa ya mabadiliko.

Lengo lao ni kuzungumzia ni ushirikiano gani wa marekebisho unaoweza kubuniwa kujenga uchumi thabiti endelevu. Mkurugenzi mkuu wa mpango huo wa GPI Ingrid Hamm, amesema kuwa bara jirani linatoa fursa katika kila sekta na linapaswa kuwa ajenda kuu ya Umoja wa Ulaya.

Ni azma yake kuifanya Ujerumani kuchukuwa majukumu zaidi katika msaada wa kimataifa na maendeleo. Hamm amesema kuwa Afrika inaimarika na kwamba karibuni bara la Afrika litaonekana kama lilivyoonekana bara la Asia miaka 30 iliyopita.

Hamm amesema kuwa lengo limewekwa katika uhuru na suluhu za Afrika. Rais wa Senegal, Macky Sall pia anunga mkono malengo hayo. Sall atalifungua kongamano hilo litakaloandaliwa kwa njia ya mtandao pamoja na Rais wa Ujerumani, Frank Walter-Steinmeier na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Biashara Duniani WTO Ngozi Okonjo -Iweala.

Mabara Ulaya na Afrika yanahitajiana

Nigeria Abuja | ECOWAS-Treffen | Macky Sall, Präsident Senegal

Macky Sall- Rais wa Senegal

Wakati wa mahojiano kabla ya janga la virusi vya corona, Sall alikiambia kituo cha televisheni cha Ujerumani cha NTV kwamba bara la Ulaya linaihitaji Afrika na Afrika pia inalihitaji bara la Ulaya. Ameongeza kwamba hawaombi msaada kwa sababu hautasaidia maendeleo ya Afrika. Amesema kwamba wanajuwa cha kufanya na kwamba wanahitaji uwezo wa kufikia masoko ya kifedha chini ya masharti nafuu.

Wito wa msaada wa kujenga viwanda, njia za reli na mfumo wa umeme unaoweza kutegemewa, pia umepata uungwaji mkono mwingi wakati wa janga la virusi vya corona. Iweala anatoa wito wa kufufuliwa kwa eneo huru la biashara na aina mpya ya utandawazi ambayo italeta pamoja masoko ya Afrika na kuyaunganisha katika mashirika yatakayoongeza thamani endelevu.

Mshirika mmoja katika kongamano hilo Mo Ibrahim, mhudumu wa simu za mkononi nchini Sudan ambaye pia ni mwanzilishi wa wakfu wa Mo Ibrahim, hivi karibuni alizungumzia kuhusu kubuniwa kwa mifumo zaidi ya uvumbuzi ya kuimarisha uchumi na kubuniwa kwa ajira baada ya janga la virusi vya corona. Kulingana na Ibrahim, amani na usalama pia ni muhimu katika mpango huu.

Pia alikuwa na matumaini kuhusu tangazo la mwezi Mei la Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kwamba mataifa zaidi tajiri yanalenga kusaidia kuimarika kwa uchumi wa Afrika kwa kutoa mabilioni ya Euro kama msaada. Macron pia anatoa wito wa kuondolewa kwa haki miliki katika chanjo kuwezesha kutengenezwa kwa chanjo barani Afrika. Ufaransa pia imefutilia mbali deni lote inayoidia Sudan.