1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Tanzania aachiwa huru

4 Machi 2022

Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Freeman Mbowe ameachiwa huru katika kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali kusema hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

https://p.dw.com/p/47zoT
Tansania Dar es Salaam Freeman Mbowe Oppositionspartei Chadema
Picha: Eric Boniface/DW

Kumekuwa na hali ya shangwe na nderemo kutoka kwa wafuasi wa chama hicho ikiwa muda mfupi baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na hivyo DPP, kuwafutia mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili.

Mbowe ambaye pamoja na washtakiwa wenzake, walikuwa leo Ijumaa waanze kutoa ushahidi wao, alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi pamoja na uhujumu uchumi makosa ambayo hayana dhamana na alikamatwa kwa mara ya kwanza wakati akiwa kwenye hekaheka ya kuendesha mikutano iliyokuwa na lengo la kuuhamasisha umma kuhusu madai ya katiba mpya.

Tansania Dar es Salaam Freeman Mbowe Oppositionspartei Chadema
Freeman MbowePicha: Eric Boniface/DW

Mmoja wa mawakili wa Mbowe, Peter Kibatala amesema ingawa safari ilikuwa ngumu, lakini angalau sasa wanaweza kupumua baada ya wateja wao kuachiwa huru.

Ameitaja kesi ya Mbowe kuwa ni moja ya mashauri magumu aliyowahi kupitia kutokana na namna ilivyogusa maslahi ya wengi

Tangu kutiwa kwake mbaroni hadi dakika hii kumekuwa na miito iliyoendelea kupaza zaidi sauti kuhusiana na kesi hiyo, huku wengi wakitaka aachiwe huru wakidai mashtaka dhidi yake yalishinikizwa kisiasa.

Wafuasi wakosoa mwenendo mzima wa kesi 

Tansania Dar es Salaam Anhänger Oppositionspartei Chadema
Picha: Eric Boniface/DW

Wafuasi wa chama hicho waliofurika kwa wingi mahakamani hapo, mbali ya kuonyesha hisia za furaha, wamekosoa namna kiongozi wao alivyotumbukia kwenye kesi hiyo.

Mbowe hajazungumza lolote makahamani hapo, lakini wakili wake amesema huenda akafanya hivyo katika siku chache zijazo.

Shinikizo la kutaka Mbowe aachiwe huru lilipata nguvu mpya katika siku za hivi karibuni na mapema mwezi uliopita, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan akimtaka atumie busara zake katika kushughulikia kesi hiyo.

Walipokutana na Rais Ikulu Dar es Salaam siku ya Jumatano, viongozi wa dini pamoja na mambo mengine waliyojadiliana naye lakini pia suala la Mbowe lilijitokeza wakisihi kuwepo kwa busara katika kushughulikia kesi dhidi ya kiongozi huyo.

Kesi ya Mbowe ilikuwa ni moja ya ajenda iliyoteka karibu maeneo yote ya nchi na kwingineko duniani, huku pia wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wakifika wakati wote mahakani hapo kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.