Kampuni za Japan zafunga viwanda China | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kampuni za Japan zafunga viwanda China

Kampuni kubwa za Japan zimefunga viwanda vyao nchini China na kuwataka raia wake wajihadhari, kufuatia maandamano ya hasira dhidi ya Japan, kuhusiana na mgogoro visiwa vya Senkaku vinavyogombaniwa na mataifa hayo mawili.

Kampuni kubwa za Japan zimefunga viwanda vyao nchini China na kuwataka wafanyakazi wake wa kigeni kubaki majumbani mwao, kufuatia maandamano ya hasira dhidi ya Japan, kuhusiana na mgogoro visiwa vya Senkaku vinavyogombaniwa na mataifa hayo mawili, ambao unatishia uhusiano wa kibiashara baina ya chumi hizo kubwa zaidi barani Asia.

Wachina wakiandamana dhid ya Japan.

Hasira mbaya zaidi za wachina dhidi ya Japan katika miongo kadhaa zilisababisha maandamano mwishoni mwa wiki na mashambulizi ya fujo dhidi ya vitega uchumi vya Japan nchini China zikiwemo kampuni za magari za Toyota na Honda, na kuwalaazimu wafanyakazi wa kigeni walioingiwa na hofu kujificha. Kufuatia hali hii, vyombo vya habari vya serikali ya China vilionya kuwa vurugu hizo zinatishia uhusiano wa kibiashara baina ya China na Japan.

Waandamanaji wakipita mbele yalango kuu la kuingilia Ubalozi wa Japan mjini Beijing.

Waandamanaji wakipita mbele yalango kuu la kuingilia Ubalozi wa Japan mjini Beijing.

China na Japan ambazo zilifanya biashara baina yao yenye thamani ya dola za Marekani 345 bilioni mwaka uliyopita, zinalumbana juu ya kundi la visiwa vidogo visivyo kaliwa vilivyoko bahari ya China Mashariki, mgogoro wa muda mrefu ambao umeripuka wiki iliyopita kufuatia hatua ya serikali ya Japan kuamua kununua baadhi yake kutoka kwa mmiliki wake, raia wa Japan. Hatua hii iliyoikasirisha China ilikuwa imelenga kuepusha kile ilichokiona kama mpango wa uchokozi zaidi wa gavana mzalendo wa Tokyo, kununua visiwa hivyo na kuvijengea.

Panasonic, Canon, Seven&I zasimamisha uzalishaji

Kampuni ya vifaa vya umeme ya Panasonic ilisema moja ya viwanda vyake kilihujumiwa na wafanyakazi wa kichina na kwamba kitaendelea kufungwa hata siku ya Jumanne, ambayo ndiyo siku ya kumbukumbu ya ulowezi wa Japan katika baadhi ya sehemu za China bara mwaka 1931. Japan inahofu kuwa siku hiyo inaweza kusababisha maandamano mengine ya vurugu dhidi yake na tayari imewaonya raia wake juu ya kutokea maandamano makubwa zaidi nchini China siku hiyo.

Kampuni ya Canon nayo imetangaza kusimamisha uzalishaji katika viwanda vyake vitatu siku za Jumatatu na Jumanne, wakati kampuni ndege ya Nippon Airways imeripoti kuongezeka kwa kukatiza kwa safari za kwenda Japana kutoka China. Kampuni ya Seven & I nayo imetangaza kufunga mamia ya maduka yake nchini China kote.

Polisi ikitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanji nje ya makao makuu ya chama tawala cha kikomunisti nchini China.

Polisi ikitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanji nje ya makao makuu ya chama tawala cha kikomunisti nchini China.

Japan yaitaka China kulinda raia wake na mali

Waziri mkuu wa Japan Yoshihiko Noda ambaye alikutana na waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta Jumatatu, ameitaka China kuhakikisha kuwa raia wake na mali vinalindwa. Panetta alisema Marekani itasimamia majukumu yake ya mkataba wa ulinzi na Japan, lakini haitaegemea upande katika mgogoro unaoendelea, na kutaka utulivu na uvumilivu kwa pande zote. Panetta aliwaambia waandishi wa habari mjini Tokyo, kuwa ni katika maslahi ya kila moja kwa Japan na China kuendeleza uhusiano mzuri na kutafuta njia za kuzuia kuongezeka kwa mgogoro huo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Japan Koichiro Gemba alisema baada ya mazungumzo na waziri Panetta, kwamba Tokyo na Washington zimekubaliana kuwa visiwa vinavyogombaniwa vimo katika mkataba wa ulinzi baina ya Japan na Marekani. China ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Japan na Japan inashika nafasi ya tatu katika washirika wa China wa kibiashara.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com