Jordan yaapa kupambana vikali na IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jordan yaapa kupambana vikali na IS

Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan ameahidi nchi yake itachukua hatua kali dhidi ya kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS, kutokana na mauaji ya rubani wake Muath al-Kasaesbeh, yaliyofanywa na kundi hilo.

Mfalme Abdullah II wa Jordan

Mfalme Abdullah II wa Jordan

Kauli hiyo ameitoa wakati ambapo Marekani imeeleza wazi kwamba iko pamoja na Jordan katika kuwaangamiza magaidi wa kundi la IS. Akizungumza na makamanda wa juu wa jeshi na maafisa wa usalama mjini Amman, Mfalme Abdullah, ameapa kuwa Jordan itaendesha mapambano makali yasiyo na huruma dhidi ya magaidi wa kundi la Dola la Kiislamu-IS, kwa sababu damu ya shahidi huyo haitapotea bure. Kasaesbeh, mwenye umri wa miaka 26, aliuawa na IS kwa kuchomwa moto akiwa hai katika kizimba.

Ameahidi mapambano na IS licha ya Jordan kuwanyonga wanamgambo wawili wa Iraq, akiwemo mfungwa wa kike mwenye msimamo mkali, Sajida al-Rishawi, ambaye wapiganaji wa IS walitaka aachiwe huru ili kubadilishana na mateka huyo wa Jordan.

Waandamanaji mjini Amman, wakiiunga mkono serikali kupambana na IS

Waandamanaji mjini Amman, wakiiunga mkono serikali kupambana na IS

Kauli hiyo ya Mfalme Abdullah ameitoa baada ya mkanda wa video kuwekwa kwenye mtandao ukimuonyesha Kasaesbeh akichomwa moto.

Kutokana na mauaji hayo, Mfalme Abdullah alikatisha ziara yake nchini Marekani na kurejea nyumbani kulihutubia taifa, ambako kumefanyika maandamano ya kutoa wito wa nchi hiyo kulipiza kisasi na hivyo kuondoa wasiwasi uliokuwepo awali wa kupambana na na kundi hilo la IS.

Marekani iko pamoja na Jordan kuiangamiza IS

Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani, nchi ambayo ni mshirika mkuu wa Jordan ameeleza wazi kwamba yuko pamoja na nchi hiyo kuliangamiza kundi la Dola la Kiislamu. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema Marekani iko pamoja na watu wa Jordan.

Psaki alisema, ''Serikali ya Jordan ni mshirika muhimu. Haya yalikuwa mauaji mabaya dhidi ya raia wa Jordan, ambayo yataifanya jumuiya ya kimataifa kujizatiti zaidi katika kuiangamiza IS. Katika suala la kuchukua hatua, bila shaka tunafahamu kuhusu adhabu ya kifo, iliyotekelezwa.''

Mfalme Abdullah akiwa na Rais Barack Obama

Mfalme Abdullah akiwa na Rais Barack Obama

Marekani inapanga kuisaidia nchi hiyo kwa kuipatia silaha za kupambana na IS. Seneta Joe Manchin, amesema Jordan inapaswa kupewa vifaa vyote muhimu vya kijeshi. Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kijeshi ya Baraza la Seneti la Marekani, Senata John McCain amesema anatarajia baraza hilo litaiidhinisha kirahisi sheria hiyo inayofaa. Aidha, ameikosoa sera ya serikali ya Rais Obama ya kupambana na IS, akisema haina mkakati kabisa.

Ama kwa upande mwingine maafisa wa usalama wa Marekani wamesema Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE, umesema utaacha kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wa IS nchini Syria, yanayoongozwa na Marekani. Maafisa hao wamesema umoja huo utaacha kushiriki kwenye kampeni hiyo ya anga baada ya ndege ya kivita ya Jordan kuanguka nchini Syria wakati wa operesheni mwezi Disemba na rubani wake kuuawa na kundi la IS.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com