IS yamchoma moto rubani wa Jordan | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

IS yamchoma moto rubani wa Jordan

Jordan imewanyonga wafungwa wawili wa kijihadi, kulipiza kisasi kwa kundi la Dola la Kiislamu IS ambalo limemuuwa rubani wa nchi hiyo kwa kumchoma moto akiwa hai.

Wajordan wakiandamana kulaani kuuawa kwa Muath al-Kaseasbeh

Wajordan wakiandamana kulaani kuuawa kwa Muath al-Kaseasbeh

Wafungwa hao wawili ambao wote ni raia wa Iraq wamenyongwa kabla ya mapambazuko, saa chache baada ya kundi la Dola la Kiislamu IS kuweka mtandaoni mkanda wa video unaomuonyesha rubani wa Jordan liliyekuwa likimshikilia mateka, akiuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.

Rubani huyo, Muath al-Kaseasbeh mwenye umri wa miaka 26, alikamatwa baada ya ndege yake kuangushwa ikiwa katika operesheni dhidi ya kundi la IS. Kuuawa kwake kumezusha ghadhabu nchini Jordan, na serikali ya nchi hiyo imeapa kuchukua kile ilichokiita ''Hatua za kuitetemesha ardhi'' dhidi ya kundi la IS. Mfalme wa nchi hiyo Abdullah II ambaye ni mshirika mkubwa wa Marekani, amekatiza ziara aliyokuwa akiifanya mjini Washington na kurejea nyumbani kutokana na hali hiyo. Mfalme Abdullah II amesema taifa taifa linaungana na familia ya rubani aliyeuawa.

Mfalme wa Jordan Abdullah II. bin al-Hussein

Mfalme wa Jordan Abdullah II. bin al-Hussein

''Leo tunasimama pamoja na familia ya shujaa wetu Muath al-Kaseasbeh na umma wetu na jeshi letu katika msiba huu ambao ni wa nchi nzima. Katika hali kama hii, ni wajimu wetu, watoto wa taifa hili kusimama pamoja na kukabiliana na mgogoro huu, ambao unatufanya tuwe na nguvu zaidi, na kuimarisha umoja wetu''. Amesema mfalme Abdullah II, kuhusiana na mauaji hayo ya kikatili dhidi ya rubani wa jeshi la nchi yake..

Wanajihadi wanyongwa kabla ya mapambazuko

Wafungwa wawili walionyingwa na Jordan ni Sajida al-Rishawi, mwanamke aliyekamatwa kuhusiana na shambulizi la kujitoa mhanga kwenye hotel moja mjini Amman mwaka 2005, ambalo liliuwa watu 60, na Ziad al-Kabouly alikamatwa mwaka 2008 akipanga mashambulizi ya mtandao wa al-Qaida nchini Jordan na Iraq.

Wananchi wa Jordan waliotoa maoni yao wamesema kuuawa kwa wahalifu hao hakutoshi kulipa kisasi kwa kifo cha mwanajeshi wao, kama anavyoeleza mmoja wao, Malik al-Maaytah kutoka mji wa Karak.

Sajida al-Rashawi, mmoja wa wanajihadi walionyongwa na Jordan

Sajida al-Rashawi, mmoja wa wanajihadi walionyongwa na Jordan

''Kunyongwa kwa Sajida hakutoshi, ni kitu kidogo ikilinganishwa na yaliyomkuta Muath al-Kaseasbeh, tunasubiri kuona makubwa zaidi yakifanywa dhidi ya kundi la IS, ambalo ni kundi la kigaidi, ambalo halina uhusiano wowote na Uislamu''.

Dunia yalaani kitendo cha IS

Pande tofauti ulimwenguni zimetoa kauli ya kuungana na Jordan baada ya kisa hicho cha kuuwa rubani wake. Rais wa Marekani Barack Obama ametoa tangazo kupitia msemaji wa Ikulu yake, akisema kifo cha rubani al-Kaseasbeh kitaimarisha dhima ya ushirika unaoongozwa na Marekani ambao unaijumuisha Jordan, katika kulipiga vita kundi la IS.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemtumia salamu za rambi rambi mfalme wa Jordan na familia ya rubani aliyeuawa, na kuyaita mauaji yake kuwa ni unyama usioelezeka. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pia amelaani mauaji ya Muath al-Kaseasbeh, akisema wauaji wake hawajali ubinadamu.

Nchini Jordan kwenyewe baadhi ya wanasiasa wameitaka nchi yao kujiondoa katika ushirika wa kijeshi dhidi ya kundi la IS, lakini serikali ya nchi hiyo imesema kisa hiki hakitateteresha ari yake ya kulipiga vita kundi hilo linalojiita Dola la Kiislamu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre

Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com