1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John McCain, gwiji wa siasa za Marekani afariki dunia

26 Agosti 2018

John McCain, mfungwa wa zamani wa kivita nchini Vietnam na seneta wa Marekani kutoka jimbo la Arizona kwa zaidi ya miongo mitatu, amefariki dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 81. Alikuwa akiugua saratani ya ubongo.

https://p.dw.com/p/33mSX
USA Senator John McCain gestorben
Picha: picture alliance/AP Photo/J. Scott Applewhite

John Sidney McCain III amekuwa na mwajiriwa mmoja tu katika maisha yake ya kipekee na ya dhoruba: Marekani. Ulikuwa utamaduni wa kifamilia. McCain alidai kuwa alikuwa dhuria wa moja kwa moja wa kapteni wa jeshi la George Washington wakati wa vita vya mapinduzi.

Na kama ilivyokuwa kwa baba na babu yake kabla yake, ambao wote walikuwa ma admiral wa jeshi wenye nyota nne kwa jina la John McCain, ametumia maisha yake yote katika utumishi wa nchi: Kwanza kama rubani wa ndege ya jeshi la majini, kisha kama mbunge hadi alipofariki Jumamosi akiwa na umri wa miaka 81, kufuatia kugundulika na saratani ya ubongo katika msimu wa kiangazi mwaka 2017.

Yeye pia angekuwa Admiral, iwapo kombora la Kisovieti la kudungua ndege halingekatisha kazi yake ya jeshi Oktoba 26, 1967. Siku hiyo akiwa kwenye operesheni yake ya 23 katika anga ya Vietnam, ndege yake chapa A-4 Skyhawk ilishambuliwa wakati ikiwa katika anga ya Hanoi.

McCain aliruka kwenye ndege hiyo kwa kutumia parachuti na kuanguka katika ziwa dogo katikati mwa mji, ambako nusura achomwe moto na kundi la watu waliokuwa na hasira. Mikono yake miwili na goti vilivunjwa vibaya.

US-Senator McCain und Ehefrau Cindy
Katika picha hii ya maktaba ya Novemba 8, 2016, seneta John McCain yuko na mke wake Cindy McCain baada ya kuzungumza mjini Phoenix.Picha: picture-alliance/AP Photo/R.D. Franklin

Baba yake akiwa kamanda wa vikosi vyote vya Marekani katika kanda ya Pacific, McCain aliendelea kuwa mfungwa wa kivita kwa zaidi ya miaka mitano. Aliachiwa mwaka 1973 baada ya makubaliano ya amani ya Paris, lakini madhara ya kimwili yaliotokana na matibabu mabaya ya maksudi ya viungo vyake vilivyovunjika -- na mateso gerezani -- vilimgharimu kazi yake ya rubani.

"Kwa sababu fulani, haukuwa muda wangu wakati huo, na ninaamini kwamba kwa sababu hiyo, nilikuwa nimepangiwa kufanya jambo," alisema katika mahojiano aliyofanyiwa mwaka 1989.

Mwanzo wa safari yake ya kisiasa

Jambo hilo, ilidhihirika wazi, lingekuwa siasa. Baada ya kuhudumu miaka michache kama kiungo wa jeshi la majini wa baraza la seneti, McCain alihamia Arizona, jimbo la nyumbani kwa mke wake wa pili, na kushinda kiti katika baraza la wawakilishi mnamo mwaka 1982. 

Malengo yake yalikua, na haraka akapanda hadi kwenye baraza la seneti, ambalo ndiyo chombo chenye nguvu zaidi kisiasa nchini Marekani. Likageuka makaazi yake ya pili kwa miaka 30. McCain kwa muda mrefu alijijengea taswira ya mpinzani wa Republican, akikaidi misimamo ya chama chake kuhusu masuala kuanzia mageuzi ya ufadhili wa kampeni hadi kwenye uhamiaji.

Hakujali sana nidhamu ya chama, mtazamo uliochochewa na matukio ya nyuma ya uasi katika maisha yake -- kama mwanafunzi mtukutu katika chuo cha jeshi la majini la Marekani, au mfungwa jeuri aliekuwa akiwachokoza wafungaji wake nchini Vietnam.

"Kunusurika kifungo changu kuliimarisha kujiamini kwangu, na kukataa kwangu kuachiwa mapema kulinifundisha kuamini katika maamuzi yangu," McCain aliandika katika kitabu cha maisha yake mwaka 1999, "Faith of My Fathers."

Vietnam John McCain
Katika picha isiyo na tarehe iliotolewa na CBS, Luteni kamanda wa jeshi la majini la Marekani John Mc cain anaonekana akiwa amelazwa baada ya kujeruhiwa kaskazini mwa Vietnam.Picha: picture alliance/AP Photo/CBS

Ni McCain huyu mwenye matata, McCain asiyedhibitika, mwenye kudharau mamlaka na wakati mwingine mwenye majigambo, aliejitosa kwenye kinyang'anyiro cha urais mwaka 2000. McCain alishindwa na George W. Bush, lakini alijiimarisha na hatimaye kuchukuwa mwenge wa chama cha Republican kutoka kwa Bush aliepoteza umaarufu.

Mwaka 2008, alifikia maridhiano na chama cha Republican, na hatimaye alishinda uteuzi wa kuwania urais kupitia chama hicho. Huku akiwa anaikaribia ikulu ya White House, alifanya uamuzi wenye utata mkubwa. Wengi wa washirika wake hawakumsamehe kwa kumteua kama mgombea mwenza wake, gavana wa Alaska asiye na uzoefu wowote Sarah Palin.

Uamuzi huo unaelezwa kuwa mojawapo ya sababu za kujitokeza kwa kundi la mashinani la Tea Party na baadae kuibuka kwa siasa kali zinazofanyiwa tashihishi na Donald Trump.

Mdemocrat Barack Obama alishinda kwa urahisi katika uchaguzi. McCain, akiwa sasa ameshindwa mara mbili, aligeukia utani kuhusu namna alivyoanza kulala kama mtoto: "Lala masaa mawili, amka na kulia, lala masaa mawili, amka na kulala."

Haiba ya John McCain

McCain alikuwa na uwezo wa kuiburudisha hadhira yake. Mjini Washington, alikuwa akizungukwa na waandishi habari katika kumbi za bunge wakati mwingine akitumia nguvu na kukosa uvumilivu. "Hilo ni swali la kijinga," alimuambia mwandishi habari aliemuuliza.

USA TV-Duell zwischen Obama und McCain 2008
Mdahalo wa televisheni - mgombea wa Republican John McCain na Mdemocrat Barack Obama, wakitabasamu wakati wa mdahalo wa pili wa wagombea urais katika chuo kikuu cha Belmot, Nashville, Tennessee, Oktoba 7, 2008.Picha: picture-alliance/ dpa/C. Berkey

Lakini wakati mwingine majibu yake ya haraka yalikuwa yakigeuka kuwa unyenyekevu: "Sidhani mimi ni mtu mwenye akili sana," alisema wakati mmoja. Wakati mwingine alikuwa akiripuka pia, hasa kuhusu mambo yenye umuhimu kwake: Vikosi vya jeshi, upekee wa Marekani na, katika miaka yake ya baadae, kitisho kinachotoka kwa rais wa Urusi Vladmir Putin, aliemtaja kuwa "muuaji na jambazi."

Wakati mwingine wenzake katika chama cha Republican walikuwa wakikejeli misimamo yake ya uingiliaji pasipo na kufikiri, wakibainisha kwamba hangeweza kusema "hapana" kwa vita. Wakati mmoja alitumia mdundo wa Beach Boys wakati akiimba kuhusu uwezekano wa "kuishambulia Iran kwa mabomu."

Kwa lengo hilo, McCain aliendelea kushawishika kwamba maadili ya Marekani yanapaswa kuzingatiwa na kutetewa duniani kote. Alikuwa akipanda ndege mara kwa mara kwenda Baghdad, Kabul, Taipei au Kiev, akipokelewa zaidi kama mkuu wa nchi kuliko mbunge.

Baada ya kuitwaa rasi ya Crimea, Urusi iliorodhesha jina lake kwenye orodha ya watu wabaya katika kujibu vikwazo vilivyoongozwa na Marekani. "Nadhani hii inamaanisha kuwa mapumzo yangu ya Siberia msimu wa machipuko yamefutwa," alijibu. Kuhusu Urusi au Syria, sauti ya McCain ilifika mbali. Lakini kiuhalisia Seneta huyo alikuwa jenerali asie na majeshi.

Kuchaguliwa kwa Donald Trump

Kuchaguliwa kwa Trump kulionekana kuvuruga mapambano na mawazo ya veterani huyo wa Republican, ambaye alikerwa na siaza za kizalendo na sera ya ulinzi ya mfanyabiashara huyo tajiri, kujikomba kwake kwa Putin na "kuuwa heshima ya ofisi ya rais." Alitofautiana pia vikali na Trump kuhusu mambo kadhaa.

USA - Senat lehnt Abschaffung von Obamacare ab
Seneta John McCain akielekea kwenye ofisi yake ya Capitol Hill kufuatia kura juu ya kubadili sheria ya bima ya afya ya Obama, maarufu "Obamacare" mjini Washington DC, Julai 26, 2017. Seneti ilipiga kura 55-45 kuikataa sheria iliyotaka kuondoa vipengele muhimu vya sheria ya Obamacare bila mpango mbadala wa kuchukuwa nafasi yake.Picha: picture-alliance/MediaPunch/CNP/R. Sachs

Lakini yote hayo hayakumfanya McCain kustafu siasa kwa furaha. Yumkini akimfikiria babu yake, aliefariki siku chache tu baada ya kurejea nyumbani kufuati kusalimu kwa Japan katika vita kuu vya pili vya dunia, McCain alitaka kusalia katika Seneti kwa kadiri awezavyo, hata wakati akikabiliwa na saratani kali ya ubongo.

Tangu Desemba 2017, hakuwa anahudhuria katika ukumbi wa seneti wakati akifanyiwa matibabu jimboni Arizona -- na aliwapokea kwenye shamba lake kubwa -- marafiki na wenzake waliokuja kumuaga mbali na vyombo vya habari.

Siku moja kabla ya kifo chake, familia yake ilitangaza kuwa alikuwa anasisitsha matibabu. McCain alifahamisha katika kitabu cha wasifu wake kilichochapishwa mwezi Mei cha "The Restless Wave" au "Wimbi Lisilotulia", kwamba angependa kuzikwa Maryland, karibu na rafiki yake wa zamani kwenye jeshi la majini Chuck Larson.

Ameacha mke Cindy na watoto saba, watatu kati yao kutoka kwenye ndoa yake ya mwanzo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Afpe, rtre.

Mhariri: Bruce Amani